HALMASHAURI
ya wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro imetoa notisi ya siku 14 kabla ya
kuchukua hatua kwa uongozi wa Chuo cha veta mikumi, Wakitaka
walipe kodi ya hoteli, “hoteli levvy’ ya shilingi milioni tano kwa
halmashauri hiyo, kutokana na kuendesha mgahawa chuoni hapo.
Mkuu
wa chuo cha VETA Mikumi, Christopher Ayo,amekiri kupokea notisi hiyo ya
Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kwa deni lililotajwa kama ni kodi ya
kipindi cha 2014 hadi 2017 lakini akafafanua kuwa mgahawa uliopo chuoni
hapo hauendeshwi kibiashara bali ni sehemu ya mafunzo kama ilivyo
kwa karakana nyingine za ufundi ukiwemo wa magari,uhunzi, umeme,
useremala, mitambo na karakana zingine ambazo zimekuwa zikiendesha
mafunzo kwa vitendo.
Amesema
bidhaa zinazotengenezwa zimekuwa zikitengenezwa kwa kutumia ruzuku ya
fedha za Serikali na wamekuwa wakiziza na mapato yake kurudi upya
Serikalini na baadaye kutumwa upya kama Ruzuku ili kusaidia chuo hicho
kuendesha kozi husika.
Ayo
amesema ni vyema wadau wa Serikali wakatambua namna mamlaka hiyo
inavyofanya kazi zake, badala ya kuchukua maamuzi bila kuwashirikisha na
kwamba baadhi ya mamlaka zingine na hata Uongozi wa wilaya uliopita
walikuwa wakitambua uendeshaji wa mafunzo katika chuo hicho na vingine
vya VETA.
Aidha
amesema katika kuboresha mafunzo ya Ukarimu chuoni hapo, Shirika lisilo
la kiserikali la With Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo la Korea
Kusini, KOIKA, wamekipatia Veta Mikumi msaada wa mashine za kisasa za
thamani ya shilingi milioni hamsini kwaajili ya kuokea mikate na vyakula
vinavyotumia unga kusaidia mafunzo kwa wanafunzi wa hoteli,utalii na
wadau wengine watakaohitaji kujifunza.
Amesema
kufuatia msaada huo, wameamua kuanzisha duka la bidhaa za Mikate na
vyakula vinavyotumia unga, ili vinunuliwe kwa bei nafuu na
wafanyabiashara wanaozunguka maeneo yao na wakiweza watumie kuuza katika
maeneo yao.
Akihimiza
umuhimu wa vijana kutumia mafunzo ya ufundi kujiajiri, Meneja
Rasilimali watu kutoka kiwanda cha Sukari cha Kilombero ambaye pia ni
mjumbe wa bodi ya wakurugenzi ya Veta Kanda ya Mashariki,Beda Marwa,
amezishauri taasisi za kifedha kutoa mikopo kwa vijana ili wapate
mitaji ya kujiajiri.
Aidha
baadhi ya wahitimu wa chuo hicho akiwemo Joyce Rafaely mkazi wa Turiani
aliyekuwa mwanamke pekee kati ya wanafunzi 43 waliokuwa wakijifunza
ufundi wa magari amesema ameamua kujikita katika kozi hiyo iliyoonekana
zaidi kufanywa na wanaume baada ya kuchungulia fursa nyingi zilizopo, na
kwamba anaamini kwa kutumia jinsia yake na ufundi uliobobea, atapata
kazi nyingi zitakazomuwezesha kuendesha maisha yake.
Mwisho.