Monday, June 24, 2013

KUTATUA MIGOGORO YA ARDHI MABWEGERE KILOSA HISTORIA YA KIJIJI INATAKIWA KUFUATWA.




Kijiji cha Mabwegere kilichopo kata ya Kitete, tarafa ya Magole wilayani Kilosa mkoani Morogoro, kimekumbwa na migogoro ya ardhi ya mara kwa mara. Peter Kimath aliyetembelea kijiji hicho hivi karibuni anaeleza sababu za migogoro hiyo.

Kijiji cha Mabwegere kipo kilomita 78 kutoka Kilosa mjini,kina ukumbwa wa hekta 10234,upande wa mashariki kimepakana na kijiji cha Mbigiri, magharibi kimepakana na kijiji cha Msowero, kaskazini kimepakana na kijiji cha Dumila na kusini kimepakana na kijiji cha Mambwega.

Mabwegere ni kati ya vijiji 164 vinavyounda mkoa maarufu wa Morogoro. Kijiji cha Mabwegere kilipewa hati ya usajili MG KIJ/522 ya 16/6/1999. Kijiji kinaundwa na vitongoji vinne, ambavyo ni  Ndagani, Ndugai, Ngoisani na Matangani, kina jumla ya wakazi 3,559,wakiwemo wanawake 1,233 na wanaume 2,326. 

Upande wa huduma za kijamii, Mabwegere kina shule moja ya msingi yenye nyumba 6 vya madarasa yakiwa pungufu kwa darasa moja. Shule ina nyumba 3 za walimu, choo cha tundu moja cha walimu na choo cha wanafunzi chenye matundu mawili. Upande wa afya hakuna Zahanati ila juhudi za wananchi za kujenga zimeanza na jengo limefikia kwenye umwagaji wa jamvi.

Eneo la kijiji cha Mabwegere lilianzishwa toka mwaka 1956. Wakati huo, eneo lilizungukwa na mashamba ya Mkonge ambayo  yalijulika na kwa majina ya Jesan Estate, Kitete Estate, Magole Estate na Msowero Estate.

Mwaka 1966 kulitokea vurugu kati ya baadhi ya wakulima na wafugaji  kutokana na tatizo la mipaka  ambalo lilimfanya Mkuu wa Wilaya wa kipindi hicho kushughulikia. Mkuu huyo aliitisha mikutano mbalimbali ambayo maamuzi yalifikiwa na kutenga rasmi eneo la Mabwegere kuwa eneo maalumu kwa ajili ya wafugaji.

Wilaya ya Kilosa ilichukua hatua hiyo ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji. Baada ya serikali kulitenga eneo hilo  kuwa la wafugaji wananchi wa Mabwegere waliamua kuiomba idara ya ardhi wilaya kulipima eneo ili wananchi waweze kumiliki kisheria.

Serikali ilikubali maombi hayo na idara husika ilifanya tathimini ya gharama za upimaji na wananchi wa Mabwegere walilipa gharama hizo na eneo likapimwa 14/12/1989. Zoezi la upimaji lilifanyika kwa kushirikiana na viongozi wote wa vijiji ambavyo vinapakana na kijiji cha Mabwegere.

Zoezi la upimaji eneo la Mabwegere na wananchi wake walikabidhiwa rasmi ramani ya eneo lao yenye No. E 149/2 iliyopewa usajili No.327558, mnamo 14/1/1990.  Kijiji cha Mabwegere kilifanikiwa kupata hati ya kumiliki ardhi yenye no.36042 ya ukubwa wa eneo la hekta 10234.

Baada ya zoezi la upimaji kumalizika viongozi wa vijiji vyote vya jirani walipewa taarifa na kufuata maamuzi ya serikali lakini hawakuwa tayari kupokea hilo.

 Viongizi wa vijiji jirani waliendelea kuuza maeneo ya Mabwegere kwa wageni kwa madai kuwa hawaitambui kama ni kijiji bali kitongoji cha Mfuru na kusababisha migogoro ya mara kwa mara. 

Katika hili viongozi wa vijiji vya Mfuru,Mambegwa,Dumila na Mbigiri wanapaswa kuunga mkono uamuzi uliofanywa na serikali wa kupima kijiji cha Mabwegere. 

Pia kuacha kabisa kulumbana kukaidi agizo la serikali ili kudumisha amani katika vijiji hivyo.

Ufumbuzi pekee wa sakata la mgogoro wa ardhi katika wilaya ya Kilosa hasa katika kijiji cha Mabwegere ni kuwaelimisha viongozi wa serikali wa vijiji husika kufuata taratibu na sheria. Viongozi hao wanatakiwa kuheshimu sheria ya matumizi ya ardhi zilizowekwa na serikali kuu.

 Ili kumaliza migogoro ya ardhi katika kijiji cha Mbwegere, serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi zinatakiwa kutoa elimu ya utawala bora na uwajibikaji kwa viongozi wa vijiji na vitongoji. Elimu hiyo itasaidia kutokana na kuonekana kuwa viongozi hao, wanachangia kwa asilimia kubwa migogoro ya ardhi kwa kupokea rushwa kutoka kwa wageni ili wawauzie ardhi.

Mwisho

                                     .
 Wananchi wakiwa na jazba kuelekea katika shule ya msingi Dumila kumsikiliza mkuu wa mkoa,Joel Bendera (hayupo pichani) baada ya kuzuka kwa vurugu za kupinga mabwegere sio kijiji ni kitongoji.

No comments:

Post a Comment