UKOSEFU WA UTAWALA BORA CHANZO CHA MIGOGORO YA ARDHI KILOSA
Na Peter Kimath
Wilaya ya Kilosa, mkoani
Morogoro imekuwa ikiandamwa na migogoro ya ardhi kwa kipindi kirefu sana ikihusisha
pande mbili za wakazi wa maeneo hayo. Mgogoro mkubwa wa kwanza ulikuwa mwaka
2000 kati ya wakulima na wafugaji wilayani Kilosa.
Kabla watu hawajasahau, Oktoba
27, 2008, mgogoro mwingine mkubwa ulizuka katika kijiji cha Mabwegere kilichopo
kata ya Kitete. Sakata hilo la ardhi lilihusisha wakulima na wafugaji ambalo
lilisababisha wakulima 832 kuwa wakimbizi katika nchi yao wenyewe.
Matatizo hayo, hayakuishia
hapo, bali yaliendelea kuwepo, ingawaje hayakuwa makubwa na kusababisha madhara
makubwa kama ile miwili ya awali.
Tafiti zilizofanywa ili kujua
kiini cha mgogoro huo wa ardhi, ziligundua
kuwa ukosefu wa sera ya uwajibikaji na utawala bora ndiyo chanzo kikubwa cha
migogoro ya ardhi katika wilaya ya Kilosa.
Tafiti zimeonyesha kuwa viongozi wengi wa
serikali za vijiji na vitongoji wamejiingiza katika sakata la kuwahujumu wananchi
wao.
Katika mgogoro wa ardhi unaoendelea
katika kijiji cha Mabwegere katika kata ya Kitete, unasababishwa na viongozi
wengi wa serikali kutokuwa na elimu ya utawala bora. Pia viongozi hao hawajua
sheria na sera zinazoongoza nchi katika utawala wa sheria ya umiliki wa ardhi
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Evarist
Tarimo anasema kuwa tatizo kubwa lililopo katika wilaya ya Kilosa ni viongozi
wa serikali za vijiji kutotambua uwajibikaji wao. Aliongeza kuwa viongozi wameshindwa
kutekeleza majukumu yao kwa wananchi wanaowaongoza hasa kwa upande wa sera na
sheria za matumizi ya ardhi.
“Mgogoro unaendelea katika
kijiji cha Mabwegere na vijiji jirani umesababishwa na baadhi ya viongozi wa
vijiji kutoka pande zote mbili za wakulima na wafugaji. Viongozi hao wametumia
madaraka yao vibaya kwa kuanza kufanya biashara ya ardhi,” alisema.
Anasema kuwa viongozi wa vijiji
vya Mabwegere, Mfuru na Dumila wamekuwa wakilumbana katika suala zima la
mgogoro wa ardhi katika kugombania mipaka. Aliongeza viongozi hao wameleta mtafaruku
katika jamii za wakulima na wafugaji kutokana na wananchi hao kutegemea ardhi
katika uzalishaji
Kwa mfano, viongozi wa vijiji
vya Mfuru na Mbigili wamekuwa mstari wa mbele kuuza maeneo ya kijiji cha Mabwegere.
Viongozi wa vijiji hivyo wamekuwa wakidai kuwa Mabwegere sio kijiji bali ni
kitongoji cha Mfuru kwa hivyo hakitambuliki kabisa kama kijiji.
Mgogoro wa kijiji cha Mabwegere
ni wa muda mrefu sana hadi kufikishwa Mahakama Kuu, ambayo ilitoa hukumu
kuwa ni kijiji cha wafugaji. Kijiji hicho kilisajiliwa kwa kufuata taratibu za
kisheria na kupewa hati namba MG/KIJ/522 ya
16/6/1999, pia kina uongozi unaojitegemea na
kutambulika na serikali.
Aliongeza kuwa vurugu
zilizotokea January 2013 katika eneo la Dumila zilisababishwa na wanachi wa
vijiji vya jirani vya Dumila, Mfuru na Mbigili waliokuwa wanapinga Mabwegere
kuwa kijiji. Mkuu wa Wilaya huyo aliongeza kuwa baada ya kutoa taarifa ya kuwa
Mabwegere ni kijiji kihalali na kinatambulika kisheria na kuwa kina uongozi
unaotambulika kisheria.
Kutokana na hali hiyo wananchi
wa vijiji vya Mfuru, Dumila na Mambegwa walijikusanya na kufunga barabara
pamoja na kuvunja nyumba za bishara maeneo ya Dumila mjini. Machafuko hayo
yalilenga nyumba ambazo zinamilikiwa na jamii ya wafugaji wanaoishi katika kijiji
cha Mabwegere kwa lengo la kushinikiza uongozi wa wilaya kubadilisha kauli.
Kufuatia vurugu hizo uongozi
wa mkoa na wilaya waliitisha mkutano wapande zote mbili na kukubaliana kuwa kwa
mujibu wa hukumu ya mahakamani ya rufaa ya kesi 53/2010, itambuliwe kuwa
Mabwegere ni kijiji halali halali.
Suala lingine ni la mahakama
ya rufaa ya kurejesha mipaka wa awali uliounda kijiji cha Mabwegere. Pia suala
la mpaka, litarudishwa kwa Jaji Mkuu ili airekebishe kwa kuingiza kipengele cha
kupitia mpaka kwa kuhusisha vijiji vyote vilivyo katika mgogoro ili kuleta
ridhaa kwa pande zote.
Suala jingine lililojitokeza
ni wakulima walionunua mashamba katika eneo la Mabwegere kupitia vijiji jirani
vya Mfuru, Mambegwa bila idhini hivyo watambuliwe na viongozi wa Mabwegere. Uongozi
wa Mabwegere uwatambue kuwa ni wanakijiji halali na waishi na kutumia ardhi kwa
mujibu taratibu na sheria.
Katika vurugu
zilizotokea kulikuwa na agenda za kisiasa kwani mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa
Morogoro, Joel Bendera kufika Dumila kuwatuliza wananchi, Mkuu wa Wilaya
alitumiwa ujumbe mfupi wa simu. Ujumbe ulimtaka atambue kwamba suala la nguvu
ya umma haliepukiki katika wilaya ya Kilosa.
Pia kumekuwepo na tatizo la
muda mrefu la viongozi wanaogombea uongozi kuweka hoja za kuwaondoa wafugaji
katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na Mabwegere kama mtaji. Jambo hilo limejenga
chuki baina ya wakulima na wafugaji na kuleta mahusiano yasiyoridhisha baina ya
jamii hizo mbili.
Tatizo kubwa zaidi lililojitokeza
ni baadhi ya viongozi katika ngazi ya vijiji na vitongoji vya jirani na
Mabwegere wanauza ardhi kinyemela bila ya kutofuata sheria. Sheria inawataka
wananchi wanaonunua ardhi kupitia Kamati ya Kijiji kukubali au kukataa kumpa
mtu ardhi ili kuepuka migogoro.
Afisa Mtendaji wa Kata ya
Kitete,Doglas Mwegalawa anasema kuwa utaratibu wa baadhi ya viongozi wa vitongoji
kuchukua majukumu ya kuuza ardhi bila kufuata utaratibu na sheria unachangia migogoro
ya ardhi.
“Mgogoro wa ardhi uliopo katika kijiji cha Mabwegere ni baada ya kijiji hicho, kupewa hati ya kuwa
kijiji, lakini vijiji vya jirani bado havikukubaliani na suala hilo na
kuendelea kuuza maeneo ya kijiji hicho,” aliongeza.
Mgogoro huo umedimiza baadhi
ya miradi ya maendeleo ya kijiji lakini kwa upande wa elimu jamii ya wafugaji
wamekuwa mstari wa mbele kuandikisha watoto shuleni wakati jamii ya wakulima ikiwa
nyuma katika suala zima la elimu.
Naye Mwenyekiti Mtendaji wa Kijiji
cha Mabwegere,Julius Lumambo anasema kuwa baada ya viongozi hao kutotambua Mabwegere kuwa kijiji bado wanaendelea kuuza maeneo ya
kijiji chetu.
Hata hivyo anasema kuwa
kinachotakiwa ili kumaliza mgogoro ni elimu ya utawala bora na uwajibikaji itolewe kwa viongozi wa vijiji na vitongoji. Lengo la kila kiongozi ni kutambua wajibu
wake katika utendaji na kuheshimu maamuzi yaliyotolewa na serikali.
Wananchi mji mdogo wa Dumila wakifunga barabara kupinga kauli ya Mkuu wa wilaya ya Kilosa,Evarist Tarimo yakidai Mabwegere ni kijiji na sio kitongoji
No comments:
Post a Comment