Friday, September 6, 2013

MAJAMBAZI YAUA MLINZI MOROGORO.

WATU watatu wanashilikiwa na Jeshi la Polisi mkoa Morogoro kwa tuhuma za kufanya  tukio la ujambazi  na wengine watatu  kukimbia  mara baada ya kumuuwa mlinzi wa kampuni ya ulinzi ya Omega walikuwa  wakilinda kwenye ghala la kampuni ya Coca Cola.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Mkoa wa Morogoro Faustine Shilogile akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 31 mwaka huu  saa 9 usiku maeneo ya Mtawala manispaa ya Morogoro.

Shilogile alimtaja mlinzi aliyeuwawa kuwa ni Elisha Simangwa Paulo (45) mkazi wa  Msamvu huku mlinzi mwenzake Otto Oscal Chakala(45) mkazi wa Chamwino kujeruhiwa vibaya sehemu ya kichwani na amelazwa katika hospitali ya mkoa wa Morogoro kwa matibabu

Alisema kuwa majambazi hao waliwavamia walinzi hao wakiwa lindoni  lakini baada ya mapambano  baina yao na walinzi na kusababisha kifo na majeruhi walitoroka  kwa kuruka ukuta na kukimbilia kusikojulikana.

Alisema polisi ilipata taarifa kutoka kwa mwananchi mwema kuwa  mmoja wa majambazi aliyejeruhiwa anatafuta usafiri kwa nia ya kutoroka,ndipo walipomkamata eneo la msamvu huku akiwa na silaha  aina ya short Gun MV 65552 ambayo walitoroka nayo kwa kumnyang’anya mlinzi.

Kamanda Shilogile alisema kuwa jambazi huyo pia alikutwa na mapanga matatu pamoja na nyundo huku Pipiki yenye namba za usajili T 169 BXM aina ya SanlG ikikamatwa kutokana na kutumika katika  tukio hilo na kwamba hakuna mali iliyoporwa katika kampuni ya Coca Cola.

Shilogile amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano na kutoa taarifa pale wanapokuwa na mashaka juu ya watu ambao hawaeleweki katika maeneo yao,na kumpongeza mwananchi aliyefanikisha kukamatwa kwa baadhi ya  majambazi hao na kwamba msako mkali unaendelea kwa ajli ya kuwapata majambazi walitoroka.
Hata hivyo Kamanda alisema kuwa wanaendelea kumhoji mtuhumiwa huyo na kupata taarifa zaidi ili kuweza kusaidia wengine kukamtwa na kuangamiza mtandao wote wa ujambazi wanaoutumia kufanya uhalifu.


Kamanda wa Polisi mkoa wa morogoro,Faustine Shilogile akionyesha waandishi wa habari hawapo pichani pikipiki iliyotumiwa katika ujambazi

No comments:

Post a Comment