Monday, November 6, 2017

CHUO CHA VETA MIKUMI CHAPEWA NOTISI

HALMASHAURI ya wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro imetoa notisi ya siku 14 kabla ya kuchukua hatua kwa uongozi wa Chuo cha veta mikumi, Wakitaka walipe  kodi ya hoteli,  “hoteli levvy’ ya shilingi milioni tano kwa halmashauri hiyo, kutokana na kuendesha mgahawa chuoni hapo.

Mkuu wa chuo cha VETA Mikumi, Christopher Ayo,amekiri kupokea notisi hiyo ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kwa deni lililotajwa kama ni kodi ya kipindi cha 2014 hadi 2017  lakini akafafanua kuwa mgahawa uliopo chuoni hapo hauendeshwi kibiashara bali ni sehemu ya mafunzo  kama ilivyo kwa  karakana nyingine za ufundi ukiwemo  wa magari,uhunzi, umeme, useremala, mitambo na karakana zingine ambazo zimekuwa zikiendesha mafunzo kwa vitendo.

Amesema bidhaa zinazotengenezwa zimekuwa zikitengenezwa kwa kutumia ruzuku ya fedha za Serikali na wamekuwa wakiziza na mapato yake kurudi upya Serikalini na baadaye kutumwa upya kama Ruzuku ili kusaidia  chuo hicho kuendesha kozi husika.

Ayo amesema ni vyema wadau wa Serikali wakatambua  namna mamlaka hiyo inavyofanya kazi zake, badala ya kuchukua maamuzi bila kuwashirikisha na kwamba baadhi ya mamlaka zingine na hata Uongozi wa wilaya uliopita walikuwa wakitambua uendeshaji wa mafunzo katika chuo hicho na vingine vya VETA.

Aidha amesema katika kuboresha mafunzo ya Ukarimu chuoni hapo, Shirika lisilo la kiserikali la With Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo la Korea Kusini, KOIKA, wamekipatia Veta Mikumi  msaada wa mashine za kisasa za thamani ya shilingi milioni hamsini kwaajili ya kuokea mikate na vyakula vinavyotumia unga kusaidia  mafunzo kwa wanafunzi wa hoteli,utalii na wadau wengine watakaohitaji kujifunza.

Amesema kufuatia msaada huo, wameamua kuanzisha duka la bidhaa za Mikate na vyakula vinavyotumia unga, ili vinunuliwe kwa bei nafuu na wafanyabiashara wanaozunguka maeneo yao na wakiweza watumie kuuza katika maeneo yao.

Akihimiza umuhimu wa  vijana kutumia mafunzo ya ufundi kujiajiri, Meneja Rasilimali watu kutoka kiwanda cha Sukari cha Kilombero ambaye pia ni mjumbe wa bodi ya wakurugenzi ya Veta Kanda ya Mashariki,Beda Marwa, amezishauri  taasisi za kifedha kutoa mikopo kwa vijana ili wapate mitaji ya kujiajiri.

Aidha baadhi ya wahitimu wa chuo hicho akiwemo Joyce Rafaely mkazi wa Turiani aliyekuwa mwanamke pekee kati ya wanafunzi 43 waliokuwa wakijifunza ufundi wa magari amesema ameamua kujikita katika kozi hiyo iliyoonekana zaidi kufanywa na wanaume baada ya kuchungulia fursa nyingi zilizopo, na kwamba anaamini kwa kutumia jinsia yake na ufundi uliobobea, atapata kazi nyingi zitakazomuwezesha kuendesha maisha yake.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment