Wednesday, October 25, 2017

KILOSA WATAKIWA KUTENGA BAJETI YA UKARABATI WA MTO


Serikali imeuagiza uongozi wa Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro kutenga fedha kila mwaka inapopanga bajeti yake kwa ajili ya dharura na ukarabati wa tuta la mto Mkondoa ili kuepusha madhara yanayotokea kwa wananchi wa Mji huo hususani wananchi wa kata ya Mbumi kipindi cha mvua.

Agizo hilo limetolewa Oktoba 22 mwaka huu na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipofanya ziara ya siku moja kujionea mwenyewe tuta ambalo linatishia uhai wa wananchi wa Mji wa Kilosa.

Waziri Mhagama amesema kila mwaka Halmashauri hiyo ihakikishe inatenga bajeti ya fedha kidogo kwa ajili ya dharura ya kukarabati tuta la mto Mkondoa na hivyo kuepusha madhara yanayoweza kuwapata wananchi wake kutokana na kubomolewa kwa tuta hilo na kusababisha mafuriko.

 “Kila mwaka Halmashauri ya Wilaya inapopanga Bajeti yake ya maendeleo ya miundombinu katika Halmashauri, hakikisheni angalau mnatenga bajeti kidogo ya ukarabati wa dharura katika tuta letu la kuokoa mafuriko kwenye mto Mkondoa, Kila mwaka hakikisheni bajeti inatengwa. Na Mhe. Diwani usikubali halmashauri ipitishe bajeti bila jambo hilo kuwepo” alisema Waziri Mhagama.

Aidha, Waziri Mhagama ameagiza Wilaya kwa nafasi yake na Mkoa kwa nafasi yao, kutumia mfumo wa maafa uliopo sasa, kukaa na kuona ni mahitaji gani yanayohitajika katika ukarabati wa tuta hilo yamo ndani ya uwezo wao na kisha kuwasilisha ofisi yake ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa katika kulikarabati tuta hilo kabla mafuriko  hayajatokea.

Pamoja na maelekezo hayo Mhe. Waziri Mhagama alilipokea ombi la Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe, katika kulifanyia kazi ombi la ujenzi wa Bwawa la Kidete lililopo Wilayani humo lililojengwa enzi za wakolni kwa lengo la kupunguza kasi ya maji ya mto Mkondoa kabla hayajafika  Kilosa  eneo ambalo huleta madhara.

Hata hivyo, Waziri Mhagama amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adamu Mgoyi na Halmashauri kwa Ujumla  kusimamia utunzaji wa tuta hilo ikiwa ni pamoja na kutunza uoto kwenye tuta hilo na wananchi kutojishughulisha na shughuli za kibinadamu kama kilimo, ufyatuaji tofali, uchomaji moto nyasi na kuwachukulia hatua wote wanaokwenda kinyume na utunzaji wa tuta hilo.

Naye Msimamizi wa ujenzi wa tuta hilo kutoka jeshi la wananchi wa Tanzania Meja YA Mgugule, amesema ili tuta la mto Mkondoa lenye urefu wa M. 4,360 na kimo cha wastani wa M. 5 liweze kufikia malengo kusudiwa, shughuli za kibinadamu kama kilimo, ufugaji, ufyatuaji tofali na nyingine pembezoni mwa tuta na mto lazima zikomeshwe mara moja. Aidha amesema iwepo dhamira ya kweli ya utuzaji wa tuta hilo na tathmini nyingine ya sehemu zilizoharibika ifanyike na zirekebishwe kabla ya mvua za masika hazijaanza kunyesha. 

Ziara ya Waziri Mhagama ya kutembelea tuta hilo imetokana na Dkt. Kebwe Stephen Kebwe Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuwasilisha ombi lake kwa Mhe. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ya Kuiomba Serikali kuchukua hatua za tahadhari za kuhakikisha tuta hilo linakarabatiwa kabla halijaleta madhara kwa wananchi.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment