SERIKALI na wadau wa maendeleo kwa kipindi kirefu imekuwa
ikishindwa kutimiza wajibu wake katika kuhudumia kundi la watoto wenye ulemavu
wa akili na viungo waliopo vijijini.
Katika kuwaokoa walemavu hakuna mkakati wowote uliowekwa kuanzia
ngazi ya kijiji hadi wilaya ya kuhakikisha watoto hao wanatambulika na kupewa
huduma zinazostahili.
Taarifa za kutoka ofisi ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri
ya Wilaya ya Mvomero, kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, kuna watoto wenye
ulemavu 88, wanaume 43 na wanawake 45. Watoto hao wenye ulemavu wapo katika
familia 48 wilayani humo.
Wakati taarifa kutoka kwa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Morogoro
inaonesha mkoa una walemavu wa viungo na akili wapatao 1563, huku
Wilaya ya Mvomero ikiwa na walemavu 13.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mvomero, Florent Kiyombo anasema
katika mipango kazi wameweka utaratibu wa kufanya sensa ya kuwatambua watoto
wenye ulemavu walioko nyumbani japokuwa utekelezaji unakwama
kutokana na ukosefu wa bajeti.
Flotent anaongeza kuwa halmashauri inashirikiana na taasisi
na mashirika binafsi ndani ya wilaya kufanya kazi ya utambuzi wa watoto wenye
ulemavu,na kutoa ushauri kwa jamii na kuangalia uendeshaji wa vituo
hivyo.
Anasema kuwa changamoto kubwa iliyopo katika familia nyingi ni
kuona aibu kuzaa mtoto mwenye ulemavu na kufikia hatua ya kumficha
ndani,kutotaka uongozi wa serikali kuwatambua na hata majirani zao
wanaowazunguka.
Pia anasema imani potofu zinachangia watoto kufichwa ndani
kutokana wengine kuona familia inapopata mtoto mwenye ulemavu si jambo la
kawaida na wanashindwa kufanya shughuli za maendeleo,mpaka wanafikia hatua ya
kuua watoto pindi anapozaliwa.
Pamoja na kuwepo watoto wenye ulemavu, hakuna shule ya watoto
wenye mahitaji maalumu katika wilaya nzima ya Mvomero.
Hali hiyo inachangia
sana watoto wengi kufichwa ndani na wazazi kukosa misaada, kushindwa kujua
sehemu ya kupata elimu ya kuwalea watoto hao, huku wilaya ikiwa na shule
za msingi 142.
Mratibu wa watoto wenye ulemavu kutoka Kijiji cha Magunga kata ya
Maskati,Estela Kasian anasema kuwa kijiji kina watoto wenye ulemavu 11,kati yao
wawili ni wenye ulemavu wa akili na viungo, ambao hawajitambui kwa
lolote.
Kasiani anasema kwa upande wake serikali ya kijiji haina utaratibu
wa kufanya sensa ya walemavu waliopo kijijini hapo,jambo linalochangia baadhi
ya familia kuficha watoto ndani na kuwakosesha huduma muhimu.
Kwa mujibu wa Kasiani katika kijiji cha Kipangilo,mama mmoja
baada ya kujifunga mtoto mwenye ulemavu ,hakutaka kumnyonyesha.
“Alipatwa na mshtuko wa kuzaa mtoto mwenye kasoro ambaye
yuko tofauti na wenzake waliotangulia kuzaliwa,” alisema Kasiani.
Kutokana na hali hiyo, mtoto yule hakupata huduma yoyote
kutoka kwa mama yake hadi anafariki kwa kuwa hakupenda watu watambue kama
ana mtoto mwenye ulemavu.,
Kasiani alisema mtoto yule alizikwa kwa siri pasipo hata
majirani kujua kinachoendelea.
“Nilisikitishwa sana kwa mtoto yule kufariki kwakuwa nilikuwa
nimeshatoa taarifa kwa viongozi wa serikali ya kijiji mama huyo apatiwe
msaada kuweza kumlea mwanae, lakini nilikosa ushirikiano wa kutosha,”anasema.
Anaiomba serikali ya wilaya kupitia wataalamu wa afya kufika mara
kwa mara sehemu za vijijini na kutoa elimu kwa jamii, kuhusu watoto wenye
ulemavu,jinsi ya kuwalea na kuacha tabia ya kukaa maofisini na kupiga soga.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Magunga,Daniel Munga anasema kuwa katika
mpango kazi wa serikali ya kijiji hakuna utaratibu wa utambuzi wa watoto
walemavu kutokana kukosa bajeti na kukosa wataalamu.
Munga anasema kuwa familia nyingi zinakuwa na dhana potofu ya
kuficha watoto ndani kutokana kukosa elimu,na hawajui pakuwapeleka.
Anasema kutokana na kukosa kipato cha kuwapeleka hospitali, wengi
wao hufichwa ndani na wengine hufariki.
Aliomba serikali kupitia wizara ya afya kuanzisha vituo vya kulea
watoto wenye ulemavu vijijini,kupeleka wataalamu wa kusaidia kundi hilo
lilosahaulika.
Ansema wakati watoto wenye ulemavu wa wa mjini wanatambulika
na kupewa msaada, waliopo vijijini wanasahaulika kabisa.
Anaongeza kuwa fedha za ruzuku zinazotolewa na Tasaf
zitolewe pia kwa familia zenye watoto wenye ulemavu kutokana na watoto
hao kushindwa kufanya shughuli za uzalisahaji na kuweza kujitegemea
wenyewe.
Mshauri wa Kituo cha kulea watoto walemavu,Eric Memorial
Foundation kilichpo Mvomero,Joseph Bakita anasimulia jinsi taasisi inavyofanya
kazi ya kusaidia familia zenye walemavu.
Wamekuwa wakitembea nyumba kwa nyumba katika wilaya ya Mvomero
kuwatambua watoto walemavu waliofichwa ndani na kuwapa wazazi elimu ya
kuwahudumia watoto,walio na hali mbaya huwachukua kuwapeleka kwenye kituo.
Anasema njia nyingine ya utambuzi wanayotumia ni kuandaa semina
kwa wazazi kwenye vijiji vyenye watoto walemavu,kuelimisha jinsi ya kulea
watoto hao,kuwapeleka watoto katika vituo vya kulea watoto walemavu.
Anaongeza kuwa watoto wengi anao walea aliwapata baada ya habari
kusambaa mtaani kuna taasisi ya kulea watoto walemavu imeanzishwa na inatoa
malezi kwa watoto wasiojiweza,wazazi husika kupewa elimu.
Mara nyingine tunatumia viongozi wa serikali za vijiji,kata na
tarafa,viongozi hao wamekuwa wakipita kila nyumba kukagua kama kuna mtoto
mlemavu na kuweza kumuandikisha na kumpeleka kwenye kituo cha kulea watoto
walemavu.
Josephine anasema changamoto kubwa wanayokutana nayo katika
kuwatambua watoto wenye ulemavu ni usafiri, kwa kuwa vijiji vya wilaya ya
mvomero viko mbalimbali na si rahisi kuvifikia hivyo kulazimu kutumia nguvu ya
ziada ili kunusuru watoto.
Anaongeza kuwa familia yenye watoto wenye ulemavu huwa
haiwathamini watoto kabisa,na hata inapotokea mtoto mwenye ulemavu anaugua
hapewi kipao mbele kupata matibabu kama mtoto mwingine asiye na ulemavu.
Anasema familia nyingi zinaona mama kujifungua mtoto mlemavu ni
mkosi kwa sababu wanategemea mtoto azaliwe akiwa amekamilika na kuweza
kuwasaidia,inapotokea tofauti wanakuwa na mshtuko na kuingiza imani za
kishirikina.
“Maeneo mengine tunapita kutoa elimu ya kuwatambua wenye
ulemavu na kupelekwa kwenye matibabu lakini viongozi wa vijiji wanapita kwa
wananchi na kutoa kauli za kuwakatisha tamaa,kusema watoto hao hawawezi
kupona,”alisema.
Anasema mtoto mwenye ulemavu wa akili anapopelekwa hospital kupata
matibu hakuna huduma maalumu ya kuwahudumia, baadhi ya madaktari
wanawabeza,wengine hutoa kauli mbaya kwa walezi wa watoto hao jambo ambalo
linatakiwa kukomeshwa ndani ya jamii.
Ameiomba Serikali ianzishe program maalumu ya kuwatambua watoto
wenye ulemavu wa akili na kuweza kupewa huduma muhimu kwani wasipotambulika
familia husika haziwajali kutokana na kuona hawana faida kwao.
Asasi zillizopo hapa nchini zinajihusisha na masuala ya walemavu,
chache zinafanya kazi zake kwa ukamilifu , wengi wanafanya kwa
mazoea, kikubwa ni kupeleka uhamasishaji, ili watoe huduma kwa ukamilifu, kwa
watendaji sharti wapate mafunzo ya hali ya juu ya kuhudumia kundi hili.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment