Tuesday, October 25, 2016

WANANCHI KIJIJI CHA DUMILA JUU KILOSA WAKABILIWA NA KERO YA MAJI NA UMEME.

WANANCHI wa Kijiji cha Dumila Juu,Kata ya Dumila Wilayani Kilosa wanakabiliwa na ukosefu wa huduma ya umeme, maji safi na salama kwa muda mrefu, hali hii inachangia wananchi kupatwa na magonjwa mbalimbali ya mlipuko.

Wakizungumza na Gazeti hili,walisema kuwa kero ya maji kijijini hapo ipo kwa muda mrefu,huku wakitumia maji ya visima ambayo sio salama kwa matumizi ya binadamu kutokana na maji hayo kutokuwa na kinga yoyote.

Christina Mwesaka alisema kuwa maji wanayotumia sio salama kwani yanachangia wakazi wengi kupatwa na magonjwa ya tumbo,kipindupindu,typhoid,wanatumia maji hayo kutokana na kukosa maji mbadala ya kutumia.

Aliiomba serikali na wahisani kujitokeza kusaidia kuweza kupata maji safi na salama,na halmashauri Kilosa kusimamia kumalizika kwa mradi wa maji wa world Bank,ambao umechukua miaka minne bila kukamilika huku wananchi hao wakiendelea kuteseka.

Adamu Chilongola alisema tatizo la umeme limekuwa kero kwa muda mrefu licha ya serikali kusambaza umeme wa REA kwa kila kijiji ila wao hawajaona umeme,wamekamilisha usambazaji wa nyanya katika nyumba zao ila umeme hawaoni,ila vijiji vya jirani vinafaidika na huduma hiyo.

“Naiomba serikali na tanesco watufikishie umeme katika kijiji chetu,tunashindwa kufanya shughuli za uzalishaji kwa kukosa nishati ya umeme.”Alisema.

Chilongola alisema kupitia uongozi wa serikali ya kijiji wameweza kujenga ofisi ya kijiji ya kisasa,ujenzi wa madarasa manne katika shule ya msingi, ujenzi wa vyoo sokoni, hivyo suala la ushirikishwaji ndilo limefanya miradi ya maendeleo kutekelezwa kwa makini.

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Kijiji,Salum Nyamunga alikiri kuwepo kwa kero ya maji safi, umeme, na kusema kuwa kero hizo ameshawakilisha kwa viongozi wa juu na wahisani mbalimbali ili kuweza kuzipatia ufumbuzi.

Nyamunga aliwataka wananchi wake kuendelea kujituma na kushirikiana katika kutekeleza miradi mbalimbali wanayoanzisha,kwani maendeleo yanaanza na mwenyeji kwanza,hivyo wasikate tama katika kuendeleza kijiji chao.


Misho.

No comments:

Post a Comment