Tuesday, October 25, 2016

POLISI WATUHUMIWA KUPIGA WAANDISHI WA HABARI KILOMBERO.

                                           


CHAMA cha waandishi wa habari mkoni Morogoro(MOROPC) kimelaani vikali kitendo cha askari polisi wilayani Kilombero kuwapiga na kuwadhalilisha waandishi wa habari wakiwa katika kutimiza majukumu yao ya kazi.

Mwenyekiti wa chama hicho, Nickson Mkilanya alisema, kitendo kilichofanywa na askari hao ni kitendo chenye kushusha hadhi na taaluma ya habari, waandishi  kupigwa na kupelekwa polisi kama watuhumiwa wengine wakati walikuwa katika harakati za kutimiza kajukumu yao ya kila siku.

“Naliomba jeshi la Polisi kufuatilia kwa makini sakat hili,na kuelimisha asakri wake jinsi ya kufanya kazi na vyombo vya habari bila kuingiliana kwani wote tunafanya kazi ya kuhumia jamii inayotunguka.”Alisema Mkilanya.


Kwa upande wake,Mhariri  wa Radio Pambazuko iliyopo wilayani Kilombero, Elias Maganga alisema jeshi la polisi linatakiwa kushirikiana na vyombo vya habari katika kutekeleza majukumu yake ili wote kwa pamoja waweze kuwahudumia wananchi na kuacha kuwa vikwazo kwa waandishi wa habari wanapotekeleza majukumu yao.

Maganga alisema kitendo cha waandishi wa habari wawili wa kituo hicho cha Radio Pambazuko kupigwa na kudhalilishwa na askari polisi wa wilaya hiyo wakati wakitekeleza majukumu yao wilayani humo ni kitendo cha unyanyasaji na hakitakiwi kufumbiwa macho kabbisa.

Maganga alisema kuwa siku ya tukio septemba 28, saa moja asubuhi waandishi, Norbert Komba na Aziza Pondamali walienda kwenye kitongoji cha Mangwale mjini Ifakara ili kuchukua na taarifa za tukio la kupigwa hadi kuuawa kwa mtu mmoja ambaye hakufahamika jina aliyedaiwa kuwa ni kibaka aliyeshambuliwa na wananchi wenye hasira kali katika eneo hilo.

Alisema, wakiwa katika eneo hilo huku wakiendelea na mahojiano huku wakiwa na kifaa cha kurekodia sauti, (tape recorder) mara walifika askari hao na kuanza kuwapiga huku wakiwahoji kuwa wamepata wapi ruhusa ya kuwahoji na kuwarekodi watu.

Alisema, baada ya kuwafanyia kitendo hicho, waliwachukua hadi kituo cha polisi na kuwalazimisha kuandika maelezo jambo ambalo waandishi hao walikataa na kuwaambia kuwa wao hawaoni sababu ya kuandika chochote sababu wao walikuwa wakitekeleza majukumu yao ya kazi.

Alisema, baada ya kuona wamekataa kuandika maelezo ndipo walipoamua kuwaruhusu kuondoka na wao kurejea ofisini na kueleza hali hiyo iliyowakuta.

Hata hivyo Maganga alisema kuwa wao kama chombo cha habari wapo tayari kuendelea kufanya kazi na jeshi hilo endapo kila upande utaheshimu na kutoingilia utendaji wa taasisi nyingine katika kuwahudumia wananchi.

Alisema, jeshi hilo linapasa kufahamu kuwa waandishi wa habari kutoka kituo hicho na vituo vingine wanafanya kazi kwa kuzingatia taaluma ya uandishi wa habari hivyo kuwaingilia katika kutekeleza majukumu yao ni sawa na kuwanyima haki yao ya msingi ya kuwahabarisha wananchi.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro Urlich Matei alisema, jeshi linafanya upelelezi wa kina kubaini askari waliohusika na tukio hilo, kufuatia kutowatambua waliohusika na tukio hilo kufuatia askari wote wa kituo hicho kukataa kuhusika wala kuwepo kwa tukio hilo.

Matei alisema, askari hakupaswa kumtoa mwandishi sehemu yake ya kazi na kumharasi kiasi hicho, hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa askari yeyote atakayebainika kuhusika na tukio hilo kwa mujibu wa kanuni za kazi.


Mwisho.

No comments:

Post a Comment