Tuesday, October 25, 2016

TUSIWAFICHE WATOTO WENYE ULEMAVU NDANI,TUWAPE HAKI ZAO ZA MSINGI.

Peter Kimath.

WAKATI Tanzania ikiwa na wizara tatu kamili zinazoshughulikia masuala ya watoto, watoto wenye ulemavu wamekuwa wakifichwa ndani na kukosa haki zao.

Wizara hizo ni pamoja na iliyopo katika Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu na ile ya Wizara ya Afya, Maendeleo yaJamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi Teknolojia na Ufundi.

Watoto hao baadhi yao wakiwa na ulemavu wa akili na viungo, wamekuwa wakifichwa katika wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro.

Kufichwa kwa watoto hao kunatokana na kule kunakoelezwa mila potofu, ukosefu wa elimu na ukandamizaji wa haki za wenye ulemavu.

 Mzee Luwi Faustine (81) mkazi wa  kijiji cha Makuyu Mvomero anasema kuwa familia nyingi tangu enzi za mababu  zilikuwa  zikiua watoto wenye ulemavu pindi wanapozaliwa. Watoto hao walikuwa wakiuawa kwa kile kinachodaiwa kuwa ni mkosi ndani ya familia.


Anasema kuwa tabia hiyo ilijengeka katika familia, kutokana na imani kuwa mlemavu sio mtu anayestahili kuishi duniani, amezaliwa na kasoro hivyo hatakiwi kuishi, kuonekana wala kujulikana na familia nyingine.


“Hakuna mtu yeyote alikuwa anatoa taarifa kuwa ana mtoto mlemavu ndani ya familia yake, kwa sababu waliogopa kutengwa. Pia waliogopa kutoshirikishwa katika shughuli za maendeleo ndani ya kijiji,”anabainisha Faustine.


Kulingana na Faustine, baada ya kubaini ubaya wa  kuua , walianza kutumia mbinu  ya kuwaficha watoto wenye ulemavu ndani, ili wasitambulike na mtu yeyote.


Anasema kuwa familia nyingi zilifanikiwa zoezi la kuficha watoto ndani na kuwaua kwa kuwa akina mama walikuwa wakijifungulia nyumbani, hivyo kuwa  vigumu kutambua  familia zilizokuwa na watoto wenye ulemavu.

Faustine anaamini kuwa  inaweza kubadilika na kuachana  na mila na desturi potofu kwa kuelimishwa, hivyo kutambua kuwa mwenye ulemavu ana haki sawa na kuishi popote huku akipata huduma zinazostahili.


Kwa upande mwingine anasema kuwa endapo kutafanyika sensa maalum kwa ajili ya wenye ulemavu vijijini, itaisaidia serikali  kuwatambu na kutoa elimu ya kumlea mtoto mwenye ulemavu pindi anapozaliwa, ili kuweza kupatiwa msaada kwa urahisi, pia itasaidia kupunguza wimbi la watoto wanaofichwa ndani.


Kwa upande wake, Dkt.Hugo Kapilima kutoka Hospitali ya SUA anasema tatizo  la mtindio wa ubongo (ulemavu wa akili) kwa watoto linasababishwa na vinasaba (Genetic), anavyokuwa ametumia mama wakati wa ujauzito, hii hutokana na kina mama kutofuata taratibu za lishe wanazopewa na wataalamu wa afya.

Dkt. Kapilima anasema kuwa  pombe na madawa ya kulevya vinakuwa na madhara makubwa, husababisha mtoto kupata tatizo linalojulikana kitaalamu kama Fetal Alcoholic Syndrome (FAS).

Anasema matumizi ya madawa ya kulevya, pombe kali, na dawa anazotumia mama wakati akiwa mjamzito, zinachangia kujifungua mtoto mwenye itilafu katika ubongo.

Pia anasema upo uwezekano mkubwa kwa mama kujifungua mtoto mwenye matatizo ya ubongo endapo atapata ajali wakati wa ujauzito.

Anasema wanawake wamekuwa na kawaida ya kutumia dawa za aina mbalimbali pindi wanapokuwa na ujauzito bila kupata ushauri wa kitaalamu, jambo linalochangia mtoto kuzaliwa na tatizo la akili.

Kijiji cha Makuyu kipo katika Tarafa ya Mvomero, Wilaya ya Mvomero, kilomita 68 kutoka makao makuu ya Wilaya,kuna watoto wenye ulemavu 48,watoto watano ni kutoka familia ya Lenat Abdallah.

Mzee Lenat Abdallah (80) mume wa  Maria Lucas (56) anasema wanalazimika kuwasidia kila kitu watoto wao watano  wenye ulemavu  wa akili na viungo.

Anasema watoto hao, wanalishwa chakula, hujisadia haja ndogo na kubwa sehemu yoyote, miguu imepinda,hawawezi kusimama na kutembea.

Kwa mujibu wa Abdallah, mtoto wake wa kwanza Charles Lenat alizaliwa mwaka 1990 akiwa hana tatizo lolote katika viungo vya mwili wake.

Anasema  kuwa alipofika umri wa miezi minne alianza kupatwa na homa za mara kwa mara na walipompeleka hospitali ya Bwagala iliyopo Turiani vipimo vilionyesha kuwa amepatwa na ugonjwa wa degedege.


Abdallah anasema kadri mtoto huyo aliyokuwa anakua akawa  hatoi sauti, kutembea wala kukaa mwenyewe, jambo hilo liliwashtua sana na walipojaribu kumpeleka hospitali hali haikubalika kabisa.


Anasema  kuwa  alipofikisha miaka tisa miguu ilianza kuvimba na mpaka sasa mwanae huyo mwenye umri wa miaka 26, hawezi kutembea,miguu imepinda, kuongea wala kujihudumia kwa lolote akiwa peke yake.


Mwanae wa pili, Severine Lenat alizaliwa mwaka 1993 akiwa mzima lakini alianza kupatwa na  homa za mara kwa mara akiwa na miezi miwili na walipomfikisha hospitali matokeo yalionesha anasumbuliwa  ugonjwa wa degedege.


Mtoto huyo alipata matibabu ya awali katika hospitali ya Bwagala, lakini walishauriwa kumpeleka hospitali ya mkoa wa Morogoro kwa matibabu zaidi. Hata hivyo, walishindwa kufanya kumpatia matibabu  kutokana na ukosefu wa fedha.


Anasema  waliendelea kuwatunza watoto wao wawili ndani bila hata majirani kujua kama watoto wao ni walemavu wa akili na viungo, kwani walikuwa wanaona ni jambo la aibu kijijini, haikuwahi kutokea  katika  familia yoyote.


Mtoto  wa tatu wa mzee Lenat Abdallah,Violet Lenat, alizaliwa mwaka 1997 akiwa mzima, lakini alipofikia  hatua ya kutembea, alianza kuumwa na walipomfikisha hospitali waliambiwa anaumwa malaria.


“Tuliendelea kupata matibabu katika hospital ya Bwagala iliyopo Turiani bila  mabadiliko yoyote. Kadri mtoto anavyokua tuliona haongei, alishindwa hata kutembea na kuanza kutambaa tu chini hali aliyonayo hadi hivi sasa,” anasema.


Mtoto wake wanne,  Emmanuel Lenat alizaliwa mwaka 2000.- Emmanuel alizaliwa mzima ila alipatwa na degedege akiwa na miezi mitatu. Tofauti na wenzake, Emmanuel  anaweza kutembea kidogo wakati wenzake waliotangulia kuzaliwa wanatambaa tu chini.


Mtoto wa tano mwenye ulemavu wa akili na viungo ni mjukuu wa mzee Lenat, Josephine Hermani. Mtoto huyo alizaliwa salama, lakini alipofikisha miezi mitatu alianza kulia hovyo na alipopelekwa hospitali kwa matibabu, hakuna msaada uliopatikana.

Anasema kuwa madkatari hawakuwa na majibu sahihi ya ugonjwa wa mtoto, kwa kuwa walishaoona ni jambo la kawaida kwa familia hiyo kuwa na watoto walemavu na kuwapa dawa za aina ya asprini kutibu homa.

Josephine aliendelea kukua katika hali ya kutokuongea, kutembea na kutojitambua kwa lolote. Mpaka sasa anaishi maisha hayo kama watoto wenzake ndani ya familia hiyo.

“Nashukuru Mungu familia haikunitenga nilipopata hawa watoto, walishirikiana nami kutafuta tiba ila ilishindikana na mpaka unavyoona hali ilivyo sasa wote wanatambaa tu chini na hawajitambui kabisa,” anasema Lenat.

Mama wa watoto hao, Maria Lucas anasema  kuwa kabla ya kukutana na mzee Lenat aliwahi kupata watoto watatu, lakini hawakuwa na matatizo yoyote, mmoja wao ni mama mzazi wa Hermani.


Kwa mujibu wa Maria kupata  watoto wenye ulemavu ni mipango ya Mungu, hawezi kumkosoa Mungu, hivyo wanaendelea kuishi na watoto wao katika hali zote bila kujali jamii inasemaje kuhusu watoto wao.


Anasema  kuwa walikuwa wanapata shida sana kijijini hapo, kwani kila mtu alikuwa anawanyooshea kidole kwa kitendo cha kuwa na watoto wenye ulemavu watano ndani, jambo hilo lilichukuliwa kwa mtazamo tofauti.


Kutokana na hali hiyo, baadhi ya familia badala ya kuwasaidia  na kuwapa ushauri, ziliwatenga na kutotoa ushikirikiano wowote kwa  familia hiyo, na kuoina ni  yenye mkosi katika eneo hilo.


Aidha anasema aliyefanya familia hiyo kutambulika na kuweza kupata misaada mbalimbali  ni Asasi ya Eric Memorial Foundation,inayojishughulisha na kulea watoto wenye ulemavu.


“Nashukuru viongozi wa taasisi hiyo,inayoongozwa na Mama Josephine Bakita, kwani imekuwa ikinishauri jinsi ya kuwalea watoto hawa”.

Dada wa watoto hao, Sesilia Lenat anasema anapata shida kuwalea ndugu zake kutokana na wazazi wao hivi sasa kuzeeka, kushindwa kuzalisha  na hakuna msaada wowote wanapata kutoka serikali.

“Ndugu mwandishi kwa siku tunakula mlo mmoja tu. Hatuwezi kwenda shambani kulima na kuacha hawa watoto wenyewe,”


“Tunaiomba serikali itusaidie kwani hawa watoto wanamahitaji kama watoto wengine wasio na ulemavu,” anasema Sesilia.

Anasema ipo haja kwa  serikali kuwa na  mipango ya kusadia kundi la wenye ulemavu wa viungo na akili waliopo vijijini ambao hawatambuliki, kuliko kuishia mijini na kuwasaidia wenye ulemavu ambao wanajiweza wenyewe hata kwa kutoa sauti.


Mwenyekiti wa Kijiji cha Makuyu, Kanurt Kikoti anakiri kuwa familia hiyo inaishi mazingira magumu sana, na kwamba inapata misaada kutoka kwa watu binafsi na taasisi za dini ambazo zinaguswa na hali ya familia hiyo.


Anasema kuwa serikali ya kijiji imejipangakuhakikisha fedha zitakazotolewa na serikali,milioni 50 za kila kijiji zilizotangazwa na Rais,Dkt.Magufuli zinawafikia wahusika,na familia zenye mahitaji maalum kupewa kipao mbele.


Kikoti anasema kuwa kila wakati wa  mavuno huwa anaitisha mkutano wa kijiji na kuwahimiza wananchi kuchangia chakula kwa ajili ya kusaidia familia mzee Lenat.


Anasema  kuwa familia hiyo kwa asimilia 90 inasaidiwa na watu binafsi wanaotoka nje ya kijiji hicho, na baadhi ya majirani wanaowazunguka. Mzee Lenat na mkewe Maria, hivi sasa wamezeeka, hivyo suala la kuwahudumia watoto wao linawapa shida sana.


Anaongeza kuwa familia hiyo inahitaji msaada mkubwa, serikali na wizara husika inapaswa kuzitupia macho familia zenye watoto wenye ulemavu pamoja na kutembelea mazingira wanayoishi vijijini.


Kwa upande wake Mshauri wa Asasi ya Eric Memorial Foundation, Josephine Bakita anasema kuwa jambo kubwa wanalolifanya ni kutoa elimu ya kuwalea watoto wenye ulemavu wilayani Mvomero.


Anasema elimu hiyo hutoa kwa kupita nyumba kwa nyumba, kuwakusanya katika kundi moja ndani ya kijiji na kuwapa elimu mara kwa mara,kutambua kundi la wenye ulemavu na kuona thamani yao.


Josephine anasema kuwa kundi la watu wenye ulemavu wa akili na viungo limetengwa, walioko vijijini hawapati huduma za shule, afya, kama wenye ulemavu walioko mijini,


“Familia ya Mzee Lenat yenye watoto watano wenye ulemavu wa akili na viungo, tumeitambulisha kwa wadau mbalimbali ambao wanatoa misaada kwao.” anasema Josephine.


Anasema kuwa serikali inapaswa kuweka mikakati ya kuwasaidia walemavu wa vijijini, kwa kuwatumia maafisa ustawi wa jamii kutembelea familia zenye watoto wenye ulemavu na kutoa elimu ya malezi.


Anasema kwa jinsi hali ilivyo, watoto wengi wenye ulemavu hawaogeshwi kutokana na wanafamilia kuwaogopa, hivyo kukumbwa na magonjwa ya ngozi.

Wakati watoto hao wenye ulemavu wakiachwa bila kuthaminiwa, ipo haja kwa wizara husika za Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu na ile ya Wizara ya Afya, Maendeleo yaJamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi Teknolojia na Ufundi, kusimama kidete kutetea maisha ya watoto wenye ulemavu.

Hakutakuwa na maana, watoto wenye ulemavu kuendelea kutaabika na kusahaulika, wakati serikali ya awamu ya tano imeunda wizara tatu, mahsusi kwa ajili yao..


Familia ya Lenat Abdallah iliyopo kijiji cha Makuyu wilayani Mvomero,familia hii ina watoto watano,wenye ulemavu wa viungo na akili.




No comments:

Post a Comment