Wednesday, October 26, 2016

TUSIWATENGE WATOTO WENYE ULEMAVU WALIOKO VIJIJINI.

Na,Peter Kimath,Morogoro.

WADAU wa Maendeleo wametakiwa kutoa  elimu ya kutosha kwa wananchi wa vijijini ili watambue watoto wenye ulemavu wana haki ya kuishi na kuhudumiwa kama wengine wasio walemavu na sio kuwaficha ndani.

Mwito huo umetolewa na Mwenyekti wa UVCCM,Morogo mjini,Salum Mkolwe, ambapo alisema  kinachosababisha wazazi kuwaficha watoto wenye ulemavu ndani ni kushindwa kuwahudumia, umaskini, pamoja na kukosa shule maalumu ya kuwapeleka, na kuona suluhisho ni kuwaficha ndani.

Alisema elimu itolewe kwa umma kwa kusimamiwa na wizara husika, namna ya kuishi na wenye ulemavu na pia kuwafundisha kuepuka unyanyapaa kwa kuwa Tanzania inaamini binadamu wote ni sawa na wanahitaji huduma zote zinazostahili.

Aidha alisema  kuwa Serikali ianzishe Kanza Data (Data Base) ambayo itawajumuisha watu wenye ulemavu wote Tanzania na kuona namna ya kuwahudumia na kuwatengea bajeti maalumu kulingana na idadi yao na mahitaji yao sehemu walipo.

Mkolwe alisema kuwa serikali ina wataalamu wengi,iwatumie kuhakikisha idadi ya watoto wenye ulemavu walioko maeneo ya vijijini,ili kuweza kutambulika na kupata msaada na sio kuziachia taasisi/mashirika binafsi kufanya hiyo kazi.

Pia alisema  miundo mbinu rafiki  itengenezwe katika kila maeneo huku ikizingatia watu wenye ulemavu, barabara maalumu za kuwajali, uwepo wa miundo mbinu rafiki katika ofisi zote za Serikali na Binafsi, na katika shule zote za serikali na binafsi.

Hata hivyo alisema kila mtu ndani ya jamii kutumia nafasi yake kusaidia kundi la wenye ulemavu,kuwapatia mahitaji yao muhimu,na kuwashirikisha katika ujenzi wa taifa,kwani wapo wenye ulemavu na wana vipaji,ila wanashindwa kuviendeleza kwa kukosa muongozo.


Mwisho.

No comments:

Post a Comment