Sunday, September 24, 2017

MKAKATI WA CoST WAJENGEA UWEZO WANAHABARI NA ASASI ZA KIRAIA



 Mkakati wa Uwazi na Uwajibikaji katika Sekta ya Ujenzi (Construction Sector Transparency Initiative – CoST Tanzania) hapo jana imeendesha Warsha ya kuwajengea uwezo Wanahabari na vikundi vya Asasi za Kiraia ili waweze kutambua hali ya ubora wa ujenzi wa miundombinu ya Umma. Washa hiyo ilifanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC).

CoST inanuia kuwatumia Wanahabari na Asasi za Kiraia kupata taarifa za ujenzi wa miundombinu, hasa katika maeneo ambayo CoST haifiki kwa urahisi, ambayo ni pamoja na Wilayani na vijijini. Taarifa zitakazotolewa zitaiwezesha CoST kufuatilia miradi hiyo kwa urahisi pale inapobidi ili kupata miundombinu bora na salama.

Katika kutekeleza azma yake, CoST imegundua kwamba Wanahabari na Asasi za Kiraia wanahitaji elimu zaidi ya kuwawezesha kutambua ubora wa miundombinu kwani wao si wataalam wa ujenzi ila kuna mambo ya msingi ambayo ni vizuri wakayaelewa ili watoe taarifa sahihi. Wanahabari na asasi za kijamii zitatumia vitini (tools) vilivyotengeneza CoST Tanzania kwa ajili hiyo.

Mwenyekiti wa CoST, Bw. Kazungu Magili ameeleza kwamba kazi kubwa ya Mkakati wa CoST ni kuendeleza uwazi na uwajibikaji katika mchakato wa ujenzi wa miundombinu ya umma. Imani ya CoST ni kwamba uwazi utapunguza maficho ya mapungufu yaliyopo kwenye sekta ua Ujenzi na hivyo kuwafanya watekelezaji wa miradi hiyo wazingatie ubora, weledi na uaminifu katika kutekeleza miradi ya Umma ya Ujenzi.

CoST ilianzishwa  mwaka 2007 huko Uingereza na kuzinduliwa rasmi 2008 Dar Es Salaam, Tanzania.  Baraza la Ujenzi la Taifa (NCC) linasimamia Mkakati huu ambao Mhimizaji Mkuu (Champion) ni Waziri katika Ofisi ya Rais, Manejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Mpaka sasa CoST imefuatilia miradi ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo miradi ya Barabara ya Nelson Mandela, Ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma na miradi mingine ambayo taarifa zake zilishatolewa kwenye matamko mbalimbali.                                                                                                                                                                                                  

Imetolewa na:
Construction Sector Transparency Initiative (CoST) Tanzania
P.O. Box 70039, Dar Es Salaam
Tel: 0739500313
Mob: 0713620232

No comments:

Post a Comment