Friday, October 13, 2017

WAKURUGENZI WAPEWA ONYO KALI


Migogoro baina ya wakuu wa wilaya,wakurugenzi pamoja na wenyeviti wa halmashauri ambayo imekuwa ikiendelea katika maeneo mbalimbali nchini na kuleta athari za kimaendeleo kwa wananchi kwa sasa imeanza kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Akizungumzia hatua hizo Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jaffo, alisema kiongozi atakayebainika kutojirekebisha pamoja na kupewa onyo zaidi ya mara mbili hatua itakayochukuliwa ni kuondolewa katika eneo alilopo.

Waziri Jaffo alisema migogoro hiyo imekuwa mtambuka katika maeneo mengi ya halmashauri hivyo wizara ya Tamisemi ikiwa ndiyo yenye dhamani imeanza kutoa mafunzo maalumu ya uongozi ili kuhakikisha viongozi hao wanafanya kazi za wananchi badala ya kuendekeza migogoro isiyoleta tija.

“Viongozi wengi baada ya kupata uteuzi walikuwa hawajapata mafunzo ya uongozi,na migogoro hiyo imekuwa ikirudisha nyuma maendeleo na waathirika wakubwa ni wananchi,”alisema

Aidha alisema migogoro hiyo inayojitokeza ni kutokana na mapungufu ya mtu mmoja mmoja katika suala la uongozi na kama wizara itafanya maamuzi stahiki endapo kunakuwa na mgogoro mkubwa kwa kushindwa kutekeleza yale aliyoelekezwa na serikali.

Waziri Jaffo hivi karibuni akiwa mkoa Morogoro alitoa maelekezo kwa halmashauri ya Wilaya ya Malinyi ambapo kulikuwa na kutoelewana baina ya ofisi ya mkurugenzi na ofisi ya mkuu wa wilaya kwa kuitaka kujirekebisha na kufanya mabadiliko kwa baadhi ya maeneo ambayo hakuyaweka wazi.

Wakati huo huo alisema kwa sasa ni kipindi cha kufanya kazi kwa uwajibikaji, nidhamu, kufanya kazi kwa juhudi, uadilifu, hivyo kuna mapungufu ambayo yamekuwa yakijitokeza kwa baadhi ya halmashauri kwa maeneo ya miundombinu ya barabara na wizara imeanza kuchukua hatua.

Alisema jambo la ubadhirifu limeanza kuchukuliwa hatua mbalimbali na Serikali na hakuna mjadala anayefanya kazi kinyume za taratibu, katibu mkuu wa wizara hiyo tayari amewachukulia hatua wahusika walioisababishia hasara Serikali katika njia moja ama nyingine.

Katika hatua nyingine Waziri Jaffo alieleza namna serikali inavyosimamia sera ya elimu kwa kufanyia ukarabati kwa shule zote za sekondari za serikali ambazo ni kongwe  kuwa za kisasa huku zikirudi katika hadhi yake na ushindani na shule nyingine hususani ya binafsi.


Alisema Serikali kupitia wizara yake ya Tamisemi itahakikisha inasimamia kikamilifu utekelezaji wa sera hiyo ya elimu kuanzaia ngazi ya awali mpaka kidato cha sita katika suala la ujenzi wa miundombinu ambalo lilikuwa limesahaurika kwa muda mrefu.
Jaffo alisema shule zipatazo 89 za serikali zinafanyiwa ukarabati ili ziwe na ubora ambao itafanya ushindani , na akaeleza kuwa shule kuwa shule 22 ambazo ni maalumu zinapewa kipaumbele.

“Nimetembelea shule ya sekondari ya wasichana ya Kilakala na shule ya sekondari ya Mzumbe ambazo ni shule maalumu,ninachowataka wanafunzi wangu msome kwa bidiii na kuhak8ikisha tunaingia katika kumi bora kitaifa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma,”alisema

Mkuu wa shule ya sekondari ya Kilakala Renalda Salum alisema kiasi cha shilingi 935.5 milioni zimetegwa kwa ajili ya ukarabati  kwenye maeneo ya mabweni 13, madarasa nane, maabara sita, bwalo la chakula, ofisi kuu, sehemu ya kufulia nguo pamoja na miundombinu ya umeme na maji.
Mwisho..

No comments:

Post a Comment