Thursday, October 5, 2017

MLEMAVU WA NGOZI AKATWA MKONO

Mzee wa miaka 75 mwenye ulemavu wa ngozi(Albino) Nassoro Msingili mkazi wa kijiji cha Nyarutanga kata ya Kisaki wilaya ya Morogoro amekatwa mkono wa kushoto na watu wasiojulikana na kutoweka nao huku watu watano wakishikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya Afisa Tarafa Lupilo wilaya ya Ulanga.

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Leons Rwegasila akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za polisi mkoani hapa alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 3 mwaka huu majira ya saa 6 usiku huko kijiji cha Nyarutanga.

Rwegasira alisema mzee Msingili akiwa nyumbani kwake amelala alivamiwa na watu wasiojulikana na kisha kumkata mkono wake wa kushoto na kukimbia nao kusikojulikana.

Alisema majeruhi huyo kwa sasa amelazwa katika kituo cha afya Dutumi na kwamba anaendelea kupatiwa matibabu na afya yake inaendelea kuimarika.
Kaimu Kamanda huyo alisema jeshi hilo kwa sasa linaendelea kuwasaka watu hao wasiojulikana na kwamba linapinga vikali mauaji na ukatili wanaofanyiwa watu wenye ulemavu wa ngozi huku likiwataka wananchi kutoa ushirikikano.

Kuhusu mauaji ya afisa tarafa Rwegasira alisema watu watano wanashikiliwa na wengine zaidi wanasakwa kuhusiana na mauaji ya afisa tarafa wa  tarafa ya Lupiro Beno Polisi wilayani ulanga mkoani morogoro aliyeuawa kikatili kwa kuvamiwa nyumbani kwake na kupigwa shoka na watu wasiojulikana.

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa morogoro Leons Rwegasira alisema bado upelelezi wa mauaji hayo ya kikatili unaendelea kufanywa na jeshi hilo la polisi, na kulaani vikali vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi kwa kufanya mauaji na ukatili kwa wengine.

Mkuu wa wilaya ya ulanga Jacob Kasema akizungumza kwa njia ya simu kuhusiana na taarifa za mauaji hayo alisema wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za mauaji hayo,na ameviomba vyombo vya sheria kuchukuoa mkondo wake mara moja.

Kasema alisema suala la mauaji kwa viongozi wa serikali katika wilaya yake halijawai kutokea hivyo,ambapo aliwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi pindi wanapoona kuna jambo ambalo hawalidhiki nalo na badala yake watoe taarifa kwa uongozi wa wilaya iki hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Naye afisa tarafa Mahenge Maliki Mlupu akizungumzia mauaji hayo alisema amesikitishwa na mauaji hayo na kuliomba jeshi la polisi kuwachukua hatua wale wote waliohusika na kifo hicho cha kikatili huku akiwataka kufikishwa mahakamani kwa haraka.

“Marehemu alikaribia kustaafu,imetuumiza kwa kiwango kikubwa sana,na tunaomba wananchi watoe ushirikiano kwa kutoa taarifa za wahusika
Katika hatua nyingine,polisi mkoani morogoro inawashikilia Iddy Juma mkazi wa Tabata Segerea na Aniset Ferdinand mkazi wa Tabata Mhang’ombe jijini Dar es salaam kwa tuhuma za kukamatwa wakisafirisha bangi viroba sita huko eneo la mizani ya Mikese,barabara kuu ya Morogoro-Dar es salaam.

Kaimu kamanda huyo alisema watuhumiwa hao walitumia gari aina ya toyota costa huku Ally Daudi mkazi wa vibandani kata ya Mbuyuni katika manispaa ya Morogoro akikamatwa na vichane 27 vya mirungi aliyokuwa ameficha kwenye mfuko wa sandarusi
Mwisho.

No comments:

Post a Comment