Wednesday, September 13, 2017

MDAHALO,BARAZA LA ARDHI NA MATUMIZI BORA YA ARDHI KATIKA KUPUNGUZA MIGOGORO YA ARDHI.

Mkazi wa Kijiji cha Newland Kata ya Mikese akichangia mada katika mdahalo ulioandaliwa na UMADEP kupitia PELUM Tanzania.

WAJUMBE WA BARAZA LA ARDHI LA KIJIJI WALILIA POSHO.

                                             


WAKULIMA wa Kijiji cha Lubungo kata ya Mikese Wilaya ya Morogoro wameiomba serikali kutunga sheria za kuwabana wafugaji pindi wanapoingiza mifugo kula mazao shambani kutokana na faini ya iliyopo  ya malipo elfu hamsini ni ndogo na haina nguvu.

Katika mkutano mkuu wa Kijiji uliofanyika wananchi hao kwa pamoja walikubaliana kupinga sheria ya fani ya elfu 50,hivyo kupeleka mapendekezo halmashauri ya wilaya kupitia baraza la madiwani kupitia upya sheria hiyo kwani haina  faida kwa mkulima anayetumia gharama nyingi shambani.

Mwito huo umetolewa katika mdahalo ulioandaliwa na shirika la UMADEP kupitia PELUM Tanzania,uliokuwa unajadili faida za baraza la ardhi la Kijiji na Mpango wa matumizi bora ya ardhi katika kutatua migogoro ya ardhi ndani ya Kijiji hicho.

Charles Luwewe alisema kuwa baraza la ardhi la Kijiji linafanya kazi kwa mujibu wa sheria,lakini tatizo la wageni kuvamia maeneo ndani ya kijiji linaendelea,na hii inatokana baadhi ya wananchi kuwaingiza ama kuingia wenyewe kwa njia za panya.

“Ndugu zetu wafugaji wana nguvu za kifedha,wanatembea na silaha kiunoni,sisi hatuna nguvu ya kupambana nao,hivyo tunaomba serikali kuwatoa wafugaji kwa kutumia sheria na adhabu ziongezwe ili wasirudi tena.”Alisema.

Kwa upande wake,Diwani wa Kata ya Mikese,Jaffar Mwega aliwataka wajumbe wa baraza la ardhi wafanye kazi kwa mujibu wa sheria,bila uonevu ama kupendelea upande mmoja kutokana na una nguvu ya fedha.

Mwega alisema atapeleka mapendekezo ya wananchi katika baraza la madiwani,pindi watakapopitia na watakachokubaliana atarudi taarifa kwa wananchi nini cha kufanya paoja na marekebisho ya sheria waliyoimba ifanyiwe marekebisho.

Pia aliwataka wafugaji wanaoingia na kuishi katika maeneo ya wakulima waondoke,na viongozi wa serikali ya kijiji kusimamia zoezi hilo,kuepuka kupokea rushwa kwa wafugaji wanaovamia maeneo ya wakulima ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara.


Mwisho.
Afisa Miradi wa UMADEP,Pesa Kusaga akiongea na wananchi wa Kijiji cha Newland kata ya Mikese.

Wednesday, September 6, 2017

WANAHABARI,RUDISHENI AMANI MVOMERO.

MKURUGENZI wa Halmashauri ya wilaya ya Mvomero Frolent Kyombo amewaomba waaandishi wa Habari wanaofanya mradi shirikishi wa utatuzi wa migogoro ya wakulima na wafugaji kupitia Klabu ya waandishi wa Habari Morogoro (MOROPC) kuandika habari sahihi zenye tija ili kuweza kuirudisha wilaya katika hali ya amani.

Kyombo alitoa mwito huo,katika uzinduzi  wa mradi huo uliofadhiliwa na The Foundation For Civil Society (FCS) na kutakiwa kufanyika katika kata za  Hembeti, Dakawa na Mvomero ambapo, alisema kuwa suala la migogoro ya ardhi limegubikwa na uwanja mpana wa jamii na kwamba upembuzi yakinifu ufanyike kabla ya kuandika habari husika.

Alisema, ikiwa wanahabari watatumia taarifa wanazokusanya na kupata majibu kwa wahusika kabla ya kuzitoa wataweza kutoa habari zitakazojenga na sio kubomoa Mvomero katika suala zima la migogoro hiyo.

Alisema, suala la migogoro ya wakulima na wafugaji wilayani humo lipo na limeshaanza kufuatiliwa kwa kiasi kikubwa na kwamba kwa ujio wa mradi huo unaohusisha wanahabari anaimani wanaweza kuwapatia suluhisho la kutibu tatizo hilo kufuatia kuwa wafukunyuzi wa mambo.

Aidha alisema, kufuatia mradi huo kuwa na lengo la kuzungumzia masuala ya Amani utasaidia jamii kuweza kuona umuhimu wa uwepo wa Amani na hivyo kufanya migogoro hiyo kupungua au kuisha kabisa.

Awali Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa Habari mkoani hapa (MOROPC) Nickson Mkilanya alisema, lengo la mradi huo nikushirikisha jamii katika kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji wilayani humo ili kurejesha amani.

Mkilanya alisema, kufuatia kuona migogoro hiyo ikishambulia katika eneo hilo zaidi licha ya kwamba eneo jingine ipo wameamua kuomba ufadhiliwa huo toka FCS na kuweza kuangalia namna ya kurejesha Amani iliyokuwepo awali ambayo sasa imeonekana kutoweka.

Alisema, migogoro hiyo katika wilaya hiyo imeweza kuleta maafa ya binadamu na wanyama na pengine kuleta athari zingine mbalimbali kwa jamii ikiwemo uharibifu wa mazao na mapigano yaliyosababisha majeruhi .

Wialaya ya Mvomero ni miongoni mwa wilaya zinakumbwa na migogoro ya ardhi mara kwa mara na kusababisha uvunjivu wa amani,hivyo wananchi kushindwa kufanya shughuli za uzalishaji zinazoweza kuwapatia kipat
Mwisho.


“KAMA NIKITENDAWILI,KIMETEGULIWA ”

 Hakuna asiyeguswa na matukio kadhaa yanayotokea sehemu mbali mbali za nchi,nimeguswa sana na tukio la watoto kutekwa huko Arusha,halafu wanapatikana wakiwa tayari wamepoteza uhai,ni tukio la kikatili sana lililofanywa na binadamu.

Tuna maswali mengi ya kujiuliza kuhusu aina ya ukatili huu uliofanywa na binadamu mwenzetu,ni nani?kwa nini afanye ukatili huu?nani kamtuma?wahusika ni wangapi?.

Jitihada zilizofanywa na familia kwa kushiriana na jeshi la polisi,pamoja na ndugu jamaa,wote walikuwa walizunguka kila pande za mji wa Arusha na nje ya mkoa kutafuta watoto Morine na Akramu,wanapatikana ndani ya shimo wakiwa tayari wamepoteza maisha…inasikitisha sana kwa ukatili huu.

Matukio yanatokea kila mara kwa nyakati tofauti,na sehemu tofauti,tunajifunza nini?nini kifanyike kuokoa watoto wetu?watoto wetu wanahitaji ulinzi wa kutosha,kila mzazi anatakiwa kuwa mlinzi hata kama mtoto sio wake.

Nakumbuka miaka ya 1990,mzazi yeyote alikuwa anawajibu wa kukuchapa viboko ukifanya kosa hata kama sio baba,mama mzazi wa mtoto mhusika,ila kwa utandawazi wa leo tamaduni hiyo imekwisha.Turudishe utamaduni wetu.

Tuwajengee uwezo wa watoto wetu kutokuwa na mazoea na mtu asiyemfahamu barabarani pindi anapotoka shuleni,mtoto akiwa shuleni mlinzi ni mwalimu,ila anapotoka shuleni mpaka kufika nyumbani mlinzi ni mzazi yeyote,tuwape ulinzi watoto wetu.

Wakati watoto Akramu na Morine wakipatikana huko Arusha wakiwa tayari wamepoteza maisha,huko Geita jeshi la polisi limemkamata kijana mmoja anayesadikiwa ndiye mhusika wa matukio ya utekaji wa watoto,”nalipongeza jeshi la polisi kwa hatua hii”

Nasema kitendawili kimeteguliwa kwa sababau mhusika mmoja tayari kajulikana,hao wengine,mtandao mzima utajulikana tu,hakuna kinachojificha chini ya jua kikaacha kuonekana,jua linamulika sehemu zote bila kufanya upendeleo wowote.

Mtazamo wa jamii,baada ya kukamatwa kijana huyo,kila mtu alitoa hukumu hata kabla ya upelelezi wa vyombo vya dola,walifanya hivyo kuonesha wamekerwa na kusikitishwa sana na ukatili waliofanyiwa watoto Akram na Morine,Roho za Marehemu zilale pema peponi…Ameni.

“hawa watoto walimkosea nini?maisha magumu ndio uteke watoto upate hela?zamu yake sasa na yeye atekwe na kupewa` adhabu,”
 
   Mwisho


Wednesday, June 28, 2017

WIZARA YA ELIMU YAJIKITA KUSAIDIA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUMU.

                                                       

SERIKALI imeanza kuboresha miundo mbinu ya wanafunzi wenye Mahitaji maalumu ikiwemo Wenye Ulemavu na Usonjo kwa kuwajengea uwezo Walimu wanaofundisha shule ya hizo maalumu pamoja na kupeleka vifaa vya kufundishia.

Tayari Serikali imeanza kutoa mafunzo kwa walimu hao 712 kutoka nchini kote ili kuboresha utalaam wao na kutoa mafunzo yatakayokidhi mahitaji ya wanafunzi ili kwenda sambamba na wanafunzi wengine.

Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Profesa Joyce Ndalichako,alisema hayo mjini Morogoro wakati akifungua mafunzo ya walimu hao kutoka mikoa ya Dar es Salaam,Pwani,Morogoro,Lindi,Mtwara na Dodoma.

Waziri Profesa Ndalichako,alisema hatua ya Serikali imekuja kufuatia kundi hilo la wanafunzi wenye ulemavu kusahulika kwa muda mrefu hatua ambayo imekuwa ikiwafanya kukosa elimu bora.

Alisema kuwa kupitia mafunzo hayo ya Walimu wanaofundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanafunzi sasa watafundishwa stadi za kazi,Mawasiliano na ufundi sahihi ili wanapohitimu kuweza kuendelea na shughuli nyingine.

Waziri Profesa Ndalichako,alisema kuwa mafunzo hayo kwa walimu yanakwenda sambamba na utoaji wa vitendea kazi vya kufundishia ambapo tayari shule 13 zimeshapatiwa vifaa hivyo .

Alisema kuwa tayari Serikali imeshaanza kufanya ukarabati wa miundombinu ya baadhi ya shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu ili kuwajengea mazingira marafiki.

Kwa upande wake,Mmoja wa walimu wanaofundisha wanafunzi hao wenye mahitaji maalumu ikiwemo ulemavu na Usonjo kutoka Kibiti,Juliana Masawe,alisema kuwa alitaka Serikali kuboresha mazingira ya wanafunzi kwakuwa wamekuwa wakisomea katika mazingira magumu.

Naye Mwalimu Mariam Khalifan Kutoka Mkoani Lindi,alitaka Serikali kuangalia namna ya kuwapatia usafiri walimu hao ili kuweza kuwatembelea na  mara kwa mara na kutoa elimu kwa  wanafunzi wanaoishi majumbani.

Aidha alitaka Serikali kutenga bajeti maalumu kwa walimu hao kwakuwa wamekuwa wakifundisha katika mazingira magumu kutokana na fedha zinazotolewa katika shule wanazofundishia zimekuwa zikipangiwa bajeti ya kununua vitu vingine


Mwisho.

VIWANDA VIPYA VYA SUKARI VIANZE NA MBEGU SAFI

WAKUIMA wa miwa  nchini wameiomba serikali kuhakikisha viwanda vipya vyote vinavyoanzishwa kwenye maeneo mbalimbali nchini kuanza na mbegu safi zinazopendekezwa na watafiti ili kupunguza tatizo na magonjwa kwenye mashamba mapya.
Kauli hiyo imetolewa kwenye maazimio ya mkutano wa watalamu wa zao (technical meeting) wakiwemo maaafisa kilimo wa viwanda vya miwa vyote,viongozi wa vyama vya wakulima wa miwa,watafiti wa zao hilo  pamoja na wadau wengine wanashughulika na zao hilo nchini.
Akisoma maazimio hayo,Mtafiti kiongozi wa zao hilo Dkt. Hildelitha Msita alisema a azimio hilo limekuja kama tahadhari kwa viwanda vinavyoanzishwa ili kuwasaidia wakulima kuondokana na magonjwa hartari ya miwa kama SMUT ambayo yanasumbua sana wakulima wa miwa kutokan na kusambaa kwake.
Alisema ugonjwa wa SMUT ni mongoni mwa magonjwa ambayo yanawasumbua sana wakulima wa nje (OUT GROWERS) na haina tiba ingawa kinga yake ni kuondoa miwa iliyoathiriwa na ugonjwa huo kwenye mashamba.
Aliongeza kuwa ugonjwa huo upo kwenye mashamba ya sasa ya wakulima viwanda vipya vinavyoanzishwa vichukue mbegu safi kutoka maabara na sio kwenye mashamba ya miwa ya sasa kwani inaweza kuambukiza tena kwenye mashamba mapya ya viwanda vipya.
Hata hivyo kwenye mapendekezo hayo wamesema endapo serikali haitasimamia vyema uanzishwaji wa vianda hivyo kwa maana ya matumizi ya mbegu bora na kuwaacha wakulima na viwanda kujichukulia mbegu mahali popote wanapotaka na kupanda mbegu wanazotaka kutasabisha viwanda vipya kukumbwa na matatizo yanayovikumba viwanda vya zamani na wakulima wadogo.
Mtafiti kiongozi wa zao hilo Dkt. Msita amesema mbegu ya NCo 376 ina uwezo wa kukabiliana na tatizo la ugonjwa huo wa SMUT na ndiyo mbegu pekee ambayo wanapendekeza mashamba mapya ya viwanda vipya yaipande kwani hata uzalishaji wake ni mkubwa na inafaa sana kwa wakulima wa nje ambao hawamwagilii kwani inastahimili ukame.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa utafiti na Maendeleo kutoka wizara ya Kilimo mifugo na uvuvi Dkt. Hussein Mansor amepongeza kazi nzuri inayofanywa na kituo cha utafiti wa miwa kibaha katika kusaidia wakulima wa miwa na kuendeleza sekta hiyo kwa ujumla na kuwataka wakulima kufuata maelekezo ya watafiti hao ili kusaidia kulima miwa kwa tija.
Dkt. Mansoor alisema  vituo vya utafiti vitaendelea kusaidia kufanya tafiti ili kupata mbegu bora zaidi ambazo zinasifa na kujibu changamoto ambazo wakulima wa zao hilo wanakabliana nazo ikiwemo magonjwa,wadudu, ukame na zingine ili kumfanya mkulima kuona tija na kuzalisha sukari inayotosheleza mahitaji ya nchi.

 Mwisho.

TOSCI WATAKIWA KUHARAKISHA UTHIBITISHAJI WA MBEGU.

WAKULIMA wa  Wilaya ya  Mbulu mkoani Manyara wameiomba Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu nchini TOSCI kuharakisha uthibitishaji wa mbegu bora wanazopelekewa na watafiti mbalimbai ili kuweza kutumika na kupata  matokeao ya  Tafiti hizo mapema.

Mwito huo umetolewa na  wakulima katika mafunzo ya shamba darasa la kilimo bora cha maharage na aina bora za mbegu za maharage zinazofanyiwa utafiti na kituo cha utafiti wa kilimo Selian Mkoani Arusha.

Mkulima Joel Fayu alisema  wamefurahishwa  na kazi nzuri inayofanywa na watafiti toka kituo hicho na kuwatafutia  mbegu bora lakini mbegu nyingi walizoziona zinafaa kwa mazingira yao na kiuchumi zote bado hazijapitishwa kuwa mbegu.

Fayu  alisema kuna mahitaji makubwa sana ya lishe kwenye familia nyingi na mbegu zenye kutatua changamoto hiyo tayari zimeshapatikana lakini zinapitia hatua nyingi hadi kuwafikia kitu ambacho wanaona kinawanyima fursa ya kumaliza changamoto hiyo kirahisi kupitia chakula.

Alisema kuwa  miongoni mwa mbegu hizo walizovutiwa nazo ni pamoja na zile zenye virutubisho vingi vya madini ya chuma,zinki na kambakamba ambazo zote wameambiwa zipo TOSCI zinasubiri kuthibitishwa na kutumika katika kilimo cha kisasa

Emannuel Beye alisema  baadhi ya mbegu za maharage kamba ndio kivutio kikubwa kwao kwenye shamba darasa hilo na zinaonekana kufaa  sana kwenye ardhi yao kutokana kulimwa kwenye eneo dogo na kuzaa zaidi huku zikiambatana na sifa nzuri za kuvumilia ukame kwani ukame na mvua chache ni tatizo kubwa wao.

Akizungumza kwa niaba ya Mweneyekiti wa halmashauri hiyo diwani wa viti maalum Ester Joel Getagno alisema  wamekuwa na ushirikiano mkubwa na kituo cha Utafiti wa Kilimo Selian katika kuwapatia wakulima mbegu bora za maharage kupitia mashamba darasa na mafunzo hali ambayo imesaidia kuongeza ari kwa wakulima kulima zao hilo.

Alisema halmashauri  itaendelea kushirikiana na watafiti hao kuweza kusaidia jitihada hizo kwa kuongeza mashamba darasa zaidi ili  kuwafikia watu wengi zaidi maana pamoja na kuinua pato la kaya na kuongeza lishe lakini pia zao la maharage linachangia kuongeza pato la Halmashauri.

Editha Nuru Mtafiti toka Kituo hicho cha utafiti Selian,Editha Nuru alisema kuwa wataendelea kuanzisha mashamba darasa hayo kila mwaka ili kusaidia kuwafundisha wakulima hao kwa vitendo kila mara bajti itakaporuhusu na mpaka sasa wana mashamba darasa 12 kwenye halmashauri ya wilaya ya Mbulu.

Alisema mpango wa upimaji udongo umeshaaza kutekelezwa kwenye maeneo mbalimbali nchi nzima na zoezi hilo litafanyika kwenye kila wilaya kuwazesha kutoa taarifa mpya za udongo na mahitaji ya mbolea na aina za mazao ya kupandwa kwenye eneo husika.

Alisema  watafiti waliopata matatizo ya kuchomwa moto na wananchi walikuwa kwenye kazi ya upimaji ardhi ambayo inaendelea kwenye maneo mbalimbali nchini kuchukua sampuli za udogo kwaajili ya kuzpeleka maabara na kuzipima ili kupata taarifa hizo.


Mwisho.
                                              
Aina mbalimbali za mbegu za maharage ambazo zinatumiwa na wakulima.

Friday, May 12, 2017

HUDUMA ZA AFYA ZAPATIKANA CHINI YA MTI




WAKATI serikali ya awamu ya tano ikiongeza bajeti ya wizara ya afya kwa mwaka 2016/2017, bado huduma za afya nchini zimeendelea kutolewa chni ya mti.

Wakazi wa Kata ya Mindu katika Manispaa ya Morogoro, wanapata huduma za afya chini ya mti kutokana na ukosefu wa jengo la zahanati na kituo cha afya.

Huduma hiyo inatolewa chini ya mti wakati sera ya Afya nchini Tanzania Afya. 2007.5.4.1  b (i) inasema”Serikali itaendelea kusogeza huduma za afya karibu na wananchi kwa kuwa na zahanati kwa kila kijiji na kituo cha afya kwa kila kata na hospitali kwa kila wilaya.”

Kata ya mindu kwa mujibu wa sensa ya 2012  ina jumla ya wakazi zaidi 8000,shule za msingi 4, zahanati 1 ya Madanganya ambayo haikidhi mahitaji ya wananchi kutokana umbali uliopo na wananchi.

                             HALI ILIVYO.
Unapofika chini ya mti uliogeuzwa kuwa zahanati, unashuhudia wakina mama wakiwa wamekaa chini na watoto mgongoni, huku wakiungua jua wakisubiri kupatiwa huduma ya kliniki kutoka kwa wahudumu wa afya.

Sanjari na wakina mama hao, wahudumu wa afya nao wako chini ya mti, wamekaa kwenye kiti na meza moja ya kutolea huduma,huku mizani ya kupima uzito watoto ikiwa imeninginizwa juu ya mti.

Huduma inayotolewa mahala hapo ni kliniki kwa watoto na elimu ya lishe. Wananchi wanafika na kutoa kadi za kliniki za watoto kwa mhudumu wa afya, na kisha huitwa jina kupatiwa huduma.

                             KILIO CHA WANANCHI.
Uchunguzi umebaini kuwa kwa miaka kumi, wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakiomba kujengewa zahanati bila mafanikio.

Mkazi wa Mindu Lysia Kanuti anasema  wamekuwa wanapewa ahadi nyingi kutoka kwa viongozi bila mafanikio.

Anasema kuwa wamekuwa wakipata huduma chini ya mti, huku wakina mama na watoto wanakaa chini, hali hii imekuwa ikijitokeza mara kwa mara lakini ufumbuzi wa changamoto hiyo hauonekani.


Kanuti  anasema wanapata huduma ya kliniki ya watoto chini ya mti kutokana na kuishi umbali wa kilomita zaidi nane kutoka zahanati ilipo.

Anaiomba halmashauri,serikali kuu,na wadau wengine wa maendeleo kuwasaidia ujenzi wa zahanati, ili kupunguza adha wanayoipata ya huduma ya afya.

“Natumia usafiri wa pikipiki kutafuta huduma za afya,ni hatari mama mjamzito kutumia usafiri wa pikipiki na baiskeli, si salama kwa afya ya binadamu.”Anasema Salome.

Salome anasema wanashindwa kufanya shughuli za uzalishaji kutokana na kutumia muda mwingi kutafuta huduma za afya, hivyo kujikuta wako nyuma kimaendeleo.

Mkazi wa Mtaa wa Lugala katika Kata ya Mindu, Hawa Hamisi anasema changamoto wanayopata katika vituo vya afya ni foleni kubwa inayotokana na upungufu wa watoa huduma katika vituo vya afya, hususani vilivyopembezoni mwa mji.

Hawa anasema usikivu wa watoa huduma umekuwa ukilalamikiwa sana, lakini hakuna ufumbuzi wa tatizo hilo, wamekuwa wakitoa kauli chafu  kwa wagonjwa, tunaomba serikali ifuatilie na kuweza kutoa adhabu kwa watakaobainika.


Pia anasema huduma ya mama na mtoto ipewe kipao mbele hususani kwenye vituo na zahanati za kata ambako ndiko kwenye watu wengi wenye kuhitaji kupatiwa huduma hiyo. Matibabu.


Anaongeza kuwa serikali ibadili utendaji wa utoaji wa huduma za afya katika zahanati, ili siku za jumamosi na jumapili utoaji wa huduma uwepo. Hiyo itasadia kupunguza foleni za wagonjwa siku za wiki.

                            
                             WATAALAMU WA AFYA.
Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Madanganya, Theresia Kilua anasema jengo la zahanati hiyo limepata ufa na uongozi wa halmashauri umewataka kutumia nyumba ya watumishi kutoa huduma za afya.

Kilua anasema imepita miezi miwili toka kuhama kwenye jengo hilo la kituo cha afya kilichojengwa kwa nguvu za wananchi kutokana na ubovu.

Anasema mazingira ya kazi ni magumu kutokana na jengo wanalotumia hivi sasa kujengwa  kwa mfumo wa nyumba ya kuishi  na sio kwa kutolea huduma za afya.

Kutokana na  mazingira ya kata ya Mindu, anasema hulazimika kupanga ratiba ya kutoa huduma ya vipimo, kliniki kwa watoto katika mitaa, na huduma hiyo inajulikana huduma ya mkoba.

Pia anasema kuwa katika kutoa huduma ya mkoba kinachofanyika ni vipimo kwa watoto, na kutoa ushauri kwa kina mama wajawazito,elimu ya lishe.
Anaongeza kuwa huduma ya mkoba inasaidia wananchi  wanaoishi mbali na vituo,kupunguza gharama za  kusafiri kutafuta huduma ya Afya.

Chini ya utaratibu huo, wamekuwa wanatoa huduma kwa wananchi zaidi ya 600 kwa siku. Huduma hiyo hufanyika mara moja kwa mwezi kwa mtaa.

Kwa upande mwingine anasema kuna baadhi ya wakina mama ni wavivu kupeleka watoto kliniki, hata wao wenyewe kufika kupata vipimo na kwamba huduma ya kuwafuata wananchi walioko mbali na vituo vya afya imewasaidia.

Theresia anasema kuwa changamoto kubwa katika zahanati ya Madanganya ni ukosefu wa maji safi na salama. Wanatumia maji ya visima pia hawana nishati ya umeme.

Mratibu wa huduma za Chanjo Manispaa ya Morogoro,Hidaya Omary anasema wanalazimika kutoa huduma ya mkoba kutokana na ukosefu wa vituo vya afya na zahanati karibu na wananchi.

Hidaya anasema watoa huduma ya mkoba katika maeneo ambayo hayana zahanati wanapewa usafiri ili kuweza kuwafikia wananchi kwa wakati.
                                 NINI KIFANYIKE.
Huduma ya Afya inapaswa kuboreshwa na kufanyika katika jengo maalumu lenye vigezo vinavyotakiwa, sio kufanyika chini ya mti na wananchi kukaa chini, jambo ambalo sio salama kiafya.


Wahudumu wa Afya waongezwe katika vituo na zahanatiza pembezoni,wapatiwe vyenzo muhimu ili kuweza kuwafikia wananchi popote walipo, pia huduma ipatikane muda wote.

Mwisho.


Monday, November 21, 2016

VIONGOZI WA KATA YA KIHONDA WATAKIWA KUTAMBUA MAJUKUMU YAO.

                                       

VIONGOZI wa kata ya Kihonda,Manispaa ya Morogoro wametakiwa kusimamimia miradi ya maendelo kikamilifu ndani ya kata,kwa lengo la kutimiza mahitaji kwa wananchi,kuepuka malalamiko ya wananchi na kutimiza ilani ya chama tawala.

Mwito huo umetolewa na Mbunge wa Jimbo la Morogoro mjini,Abdulaziz Abood wakati akiwa katika ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo na kujua kero za wananchi ndani ya manispaa hiyo.

Abood alisema haitapendeza viongozi kuwepo ofisini,huku wananchi wakiendelea kulalamika hakuna huduma za kijamii na hakuna hatua zozote zinazochakuliwa.

Alisema kuwa kata ya kihonda inasumbuliwa sana na kero ya maji ila tayari wameshapata ufadhili kutoka nchini Ufaransa watakaowekeza kiasi zaidi ya milioni 40 katika mradi wa maji katika manispaa hiyo.

“tatizo la maji litakwisha,serikali ya awamu ya tano tumejipanga vizuri,hata bungeni nilisema tatizo hili la maji na tayari linafanyiwa kazi kwa kina.”Alisema.

Nao wakazi wa kata hiyo,walimpongeza Mbunge Azizi kwa jitihada anazofanya za kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu hasa za maji,elimu na Afya.

Hata hivyo walisema wako tayari katika kuchangia shughuli  za maendeleo ya kata yao,na kuomba serikali kuangalia sakata la barabara na upatikanaji wa dawa katika zahanati ya kata.



MAGONJWA YASIYO YA KUAMBUKIZA TISHIO NCHINI

SERIKALI imesema kufikia 2030 itapunguza 1/3 ya vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa kukinga,kutibu,kuzingatia afya ya akili na kuboresha huduma za kinga na tiba ya utumiaji wa madawa ya kulevya na pombe.

Pia kufikia 2020,imejipanga kupunguza ½ ya idadi ya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani,zinazotokana na wananchi kutotii sheria za barabarani.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Watoto,Dr.Magreth Mhando katika mkutano wa utekelezaji wa huduma za NCD ngazi ya mikoa na wilaya kuhusu magonjwa yasiyo kuambukiza.

Dr.Magreth alisema kuwa pamoja na rasilimali chache zilizopo Tanzania imepiga hatua katika kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza,licha ya kuongezeka kwa kasi katika nchi zilizoendelea ikiwemo Tanzania.

Alisema kuwa ulifanyika na Wizara ya Afya,maendeleo ya jamii,jinsia,wazee na watoto kwa kushirkiana na shirika la Afya duniani na NIMR inaonesha viashairia vya magonjwa yasiyo ya kuambukiza kuongezeka.

Alisema idadi ya watu wanaovuta sigara ni 15.9%,wanaokunywa pombe ni 29.3%,wenye uzito uliopita kiasi 34.7%,shinikizo la damu 25.9% nawagonjwa wa kisukari 9.1%.

Kwa upande wake,Kaimu Mkurugenzi Msadizi wa Magonjwa yasiyo kuambukiza kutoka Wizara ya Afya,Shadrack Dusweli alisema lengo la kutano ni kuweka mikakati kwa kushirikiana na wataalamu wa afya kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Dusweli alisema vitu vinavyosababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni mtindo wa maisha,unywaji pombe,uvutaji wa sigara,ulaji wa hovyo,madawa ya kulevya  pamoja na kutofanya mazoezi.

Pia alisema wameweka mikakati ya kupunguza magonjwa hayo kwa kushirikiana na jamii,kuongeza wataalamu,kuteua wataalamu kila mkoa na wilaya,na tarehe 17/12/2016 itazinduliwa kampeni rasmi ya upimaji wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza hapa nchini.



MAAFISA ARDHI CHANZO CHA MIGOGORO YA ARDHI

                                             
Diwani wa kata ya Mkuyuni wilaya ya Morogoro,Mwinyi Buyi akichangia mada katika mdahalo wa kujadili njia za kupunguza migogoro ya ardhi,ulioandaliwa na UMADEP kupitia PELUM-Tanzania.

Mwamasishaji kutoka Chuo cha SUA,Emmanuel Malisa akionge na wananchi wa kijiji cha Mfumbwe kilichopo katika kata ya Mkuyuni wilaya ya Morogoro,jinsi ya kupunguza migogoro ya ardhi.


Mkazi wa Kijiji cha Luholole kilichopo kata ya Mkuyuni,wilaya ya Morogoro,Ramadhani Makangira akichangia mada katika mdahalo wa kujadili njia sahihi za kupunguza migogoro ya ardhi ulioandaliwa na UMADEP kupitia PELUM-Tanzania.


WANANCHI  wa Kijiji cha Luholole na Mfumbwe vilivyopo tarafa ya Mkuyuni Wilaya ya Morogoro, wameitupia lawama lawama ofisi ya Ardhi, mipango miji na vijiji Wilayani humo,wakidai imekuwa chanzo cha migogoro ya mipaka baina Kijiji kimoja na kingine.


Madai hayo yameibuka kijijini hapo katika katika  mdahalo  ulioandaliwa  na shirika lisilo la kiserikali  la Uluguru Mountains Agricultural Development Project (UMADEP) kupitia PELUM Tanzania,uliokuwa unajadili kuhusu nini kifanyike kumaliza migogoro  ya ardhi vijijini.

Walisema  kama hali itendelea hivyo na hatua za haraka hazitachukuliwa    katika kuzuia migogoro ya mipaka baina a Luholole,Mfumbwe,Madami, inaweza kutokea migogoro mikubwa ya ardhi kwa makundi ya watu waliopo wilayani humo.

“Migogoro mingi ya ardhi mkoani Morogoro, imetokana na baadhi ya viongozi wa mkoa na wilaya, kuamua kuanzisha na kupima vijiji vipya bila kuhusisha viongozi wa vijiji husika, na matokeo yake kusababisha mvutano baina ya vijiji hivyo, na hata kupelekea uvunjifu wa amani.”alisema Shiwi Chalo kutoka kijiji cha   Luholole.

Mkazi wa kijiji  cha Mfumbwe ,Ashura Juma alisema  kuwa wananchi  wanailalamikia  ofisi  ya ardhi  na watendaji wake   kutokana na kuamua  kufanya  maamuzi  ya  kugawa vijiji  wakiwa  maofisini  bila  ya kuwashirikisha  wananchi husika  katika  vijiji .
Alisema  kuwa  hali hii itaendelea kujitokeza katika wilaya ya Morogoro, kama  ofisi  ya ardhi  haitabadili  mfumo wa  kutoa maamuzi  bila  kushirikisha  wananchi  kwenye  vijiji husika.


Afisa mipango miji na vijiji wilaya ya Morogoro, Andrea Biashara alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo,na kuahidi kuzifanyia kazi na kuwataka wananachi wa vijiji husika kukaa meza moja na kukubaliana kabla ya wataalamu wa ardhi kushirikishwa.


Kwa upande  wake Mhadhiri  wa chuo  kikuu cha kilimo( SUA), Emanuel Malisa aliwataka viongozi wa serikali ya vijiji , kushirikiana  na  kamati  za usuluhishi ,mabaraza  ya  ardhi  na  watalaam  wa ardhi  katika  kutatua  migogoro  yao  ili kudumisha amani .


PELUM kwa kushirikiana na UMADEP wako katika utekelezaji wa mradi wa CEGO ambao unaendesha midahalo katika vijiji vya  wilaya za Morogoro na Mvomero, midahalo ambayo ina lengo la kujadili namna nini kifanyike kupunguza migogoro ya ardhi.

Mwisho.

Sunday, November 6, 2016

SANAA IMENIFANYA KUKUBALIKA KATIKA SIASA.

                                                       
Mwenyekiti wa Kijiji,Dumila Juu,Kilosa,Salum Nyamunga akikagua ujenzi wa shimo la choo cha ofisi ya Kijiji.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Dumila Juu,Kilosa,Salum Nyamunga (Msanii Bazgar) akionesha ujenzi wa ofisi ya kisasa ya kijiji unavyoendelea.

WASANII wa filamu,waimbaji Bongo Flavour,taarabu,wamejiingiza kwenye siasa, na hii inatokana na kuona usanii wao unaweza kuwabeba na kujiaminisha kwa wananchi ili kuwachagua na kuwaongoza.

“napenda sanaa, muziki wa Bongo Flavour kwani ndio imenifanya kuingia kwenye siasa na kuweza kukubalika na wananchi wengi, na kunipa nia ya kuwaongoza.”Haya ni maneo ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Dumila juu,Kilosa,Morogoro,Salum Nyamunga.

Nyamunga ni Msanii wa Bongo Flavour,anayetamba na kibao cha “NIPO”,pia ni mwenyekiti wa Kijiji cha Dumila Juu,kichopo Wialayani Kilosa mkoani Morogoro.

Salum Nyamunga anasema alianza harakati za siasa mwaka 2012 kwa kutumia sanaa, alikuwa anatumia sanaa kuhamasisha sana,alikuwa akiona mikutano ya kisiasa hudhuria na kupanda jukwaani.

“nilipanda jukwaani na kuaimba nyimbo za kukosoa jamii,hasa viongozi wanaopewa madaraka na kusahau wale wananchi waliowapigia kura na kuwepo madarakani”Anasema.

Salum anasema alitumia wimbo wake unaojulikana kwa jina la “Karibu Jimboni,wimbo huo unawakumbusha viongozi kutimiza ahadi zao,warudi jimboni na sio kuimbilia mijini na kutotimiza walicho ahidi kwa wananchi kipindi cha kampeni.

Anasema wimbo mwingine uliompa sifa na kuweza kuingia kwenye siasa,”Mnazingua”, wimbo huu unaikosoa vingozi wa serikali ya kuondokana na rushwa,kutojiingiza kwenye mikataba hewa inayoingizia serikali hasara ya mabilioni ya fedha huku wananchi wa chini wanateseka kwa kukosa huduma.

Anaongeza kuwa kilichomfanya hasa kujiingiza kwenye siasa,lengo likiwa nikuwasaidia wananchi kuweza kuondokana na kero za hapa na pale,pia kuona baadhi ya viongozi wanashindwa kutambua dhamana waliyopewa na wananchi.

Pia anasema kipindi alipoanza kupiga kampeni za kugombea nafasi ya mwenyekiti wa kijiji,hakuwahi kutoa ahadi yoyote kwa wananchi wake,alichokuwa anaema ni kudumisha ushirikishwaji katika nyanja zote za maendeleo ndani ya kijiji.

Anaongeza kuwa wananchi wake wamejenga uaminifu kwa wasanii sana,wakiingia kwenye siasa wanaweza kupaza sauti,wanaweza kujiaminisha sana,waadilifi na waaminifu ndio maana wengi waliopewa madaraka wameweza kuwajibika.

“Tuna wasanii wengi wanasiasa na wanafanya kazi, kuna Profesa J,Mbunge wa Mikumi,Mbunge wa Mbeya mjini,Mbilinyi,wamekuwa mfano mzuri kwenye tasnia yetu ya sana na matunda yao yanaonekana kwa wananchi waliowapa dhamana.”Anasema.

Salum Nyamunga,anayejulikana na kwa jina la kisanii,”Bazgar” anasema nia yake ya kutumia sanaa katika siasa imemsadia sana kutoa elimu mbalimbali katika jamii,na wananchi wa Dumila wamebadilika sana kupitia uongozi wake.

Anasema nyanja nyingine wanayotumia wasanii kuingia kwenye siasa,ni kujiamini,anaamini anavyokubalika katika nyimbo zake,zinavyopendwa,ndivyo hivyo atatumiamaneo ya kisanaa jukwaani kujiaminisha kwa wananchi.

Anaongeza kuwa kazi ya sanaa ni kazi kama nyingine,tusimhukumu msanii kutokana na mavazi yake,ama matendo yake,tuangalie anatengeneza nini cha kuijenga jamii inayomzunguka,tuangalie uwezo wake wa kufikiri na kutathimini mambo.

Mweyekiti,Salum anasema kazi za serikali zipo kwenye mpango mkakati,ratiba maalumu na zinatambulika zinafanyika wakati gani na eneogani,hivyo hupanga muda wake na kuweza kutimiza ratiba yake bila kuingiliana.

“ratiba zangu hazimkwazi mtu yeyote, kuna muda wa kwenda studio kutengeneza nyimbo, kuna muda wa kuhudumia jamii, kuna muda wa vikao,mimi nakwenda kwa ratiba na kutimiza kila jambo kwa wakati.”Anasema Bazgar.

Anasema changamoto anayokuta na nayo ni pale anapopanga ratiba ya kufanya shoo mkoani,halafu inatokea shughuli za kiserikali kutoka kwa viongozi wa juu,wilayani ama mkoani,hapo inabidi kuchagua moja la muhimu na kuacha lingine.

Pia anasema anaongoza wananachi wake kwa kutumia mahusaiano (ushirikishwaji),hii inamsaidia sana kuweza  kutimiza jukumu lake kama kiongozi,kila mwananchi anashirikishwa kwa njia tofauti katika miradi ya maendeleo.

Aliingia kwenye kugombea nafasi ya mwenyekiti wa Kijiji cha Dumila 2014,alipita kwa kishindo katika hatu zote,na hiyo ilitokana na kujiaminisha kwa wananchi kwa kutumia sanaa,nyimbo za bongo flavuor anazo tunga na kuimba.

Nyamunga anasema kuwa toka alipochaguliwa kuongoza kijiji hicho,kwa kushirikiana na wananchi wake wameweza kujenga ofisi ya kisasa ya serikali ya kijiji,kujenga vyoo katika gulio wanaolotumia.

Miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa madarasa 4,pamoja na nyumba ya mwalimu katika shule ya msingi Dumila,ambapo hapo awali wanafunzi zaidi ya 1521 kuanzia darasa la awali walikuwa wanatumia vyumba 7 tu.

Msanii Bazgar anasema kiongozi yeyote ukitaka kufanikiwa katika uongozi wake, kujiamini katika utendaji, kuwashirikisha wananchi kila jambo unalofanya, kukubali ushauri wa wananchi,wazee,na viongozi waliokutangulia,hiyo ndio dhana yauongozi bora na sio bora kiongozi.

Anasema licha ya kijiji hicho kukabiliwa na ukosefu wa maji safi na salama, umeme,bado wako imara katika kuimarisha miradi ya maendeleo,kuthibiti mapato ya ndani ya kijiji,na kero hizo zimeshafikishwa kwa walengwa na zitapatiwa ufumbuzi mapema.

Mwenyekiti na Msanii,wa bongo flovour,Bazgar hivi sasa anatamba na kibao cha “nipo”,kikiwa na lengo la kuwaambia mashabiki wake bado yupo kwenye muziki na sio kapotelea tu kwenye siasa.

Bazgar amewahi kutamba na nyimbo ya “Kilosa”,iliyokuwa inahamasisha kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji Kilosa,nyimbo nyingine ni Mnazingua,Karibuni Jimboni na Umemkosa.

Hata hivyo anasema katika tasnia ya sanaa,kuna mambo mawaili,msanii kujimiliki ama kumilikiwa,hii inatokana uamuzi wa msanii mwenyewe,kwani kila mtu ana mtazamo wake katika sanaa na atapata faida gani kupitia sanaa anayofanya.

Pia anasema lengo lake ni kuendeleakuwepo katika kuongoza jamii,ataendelea kugombeanafasi mbalimbali za kisiasa zinajitokeza.

Anawataka wasanii kutumia sanaa katika kusaidia jamii,na wale wenye vipaji vya kuongoza/kuwania uongozi wasisite,watumie nafasi kwani wananchi wanajiaminisha sana kwa msanii akipewa madaraka.


Mwisho.