WAKATI serikali ya awamu ya tano ikiongeza bajeti ya wizara ya
afya kwa mwaka 2016/2017, bado huduma za afya nchini zimeendelea kutolewa chni
ya mti.
Wakazi wa Kata ya Mindu katika Manispaa ya Morogoro, wanapata
huduma za afya chini ya mti kutokana na ukosefu wa jengo la zahanati na kituo
cha afya.
Huduma hiyo inatolewa chini ya mti wakati sera ya Afya nchini
Tanzania Afya. 2007.5.4.1 b (i) inasema”Serikali itaendelea kusogeza
huduma za afya karibu na wananchi kwa kuwa na zahanati kwa kila kijiji na kituo
cha afya kwa kila kata na hospitali kwa kila wilaya.”
Kata ya mindu kwa mujibu wa sensa ya 2012 ina jumla ya
wakazi zaidi 8000,shule za msingi 4, zahanati 1 ya Madanganya ambayo haikidhi
mahitaji ya wananchi kutokana umbali uliopo na wananchi.
HALI ILIVYO.
Unapofika chini ya mti uliogeuzwa kuwa zahanati, unashuhudia
wakina mama wakiwa wamekaa chini na watoto mgongoni, huku wakiungua jua
wakisubiri kupatiwa huduma ya kliniki kutoka kwa wahudumu wa afya.
Sanjari na wakina mama hao, wahudumu wa afya nao wako chini ya
mti, wamekaa kwenye kiti na meza moja ya kutolea huduma,huku mizani ya kupima
uzito watoto ikiwa imeninginizwa juu ya mti.
Huduma inayotolewa mahala hapo ni kliniki kwa watoto na elimu ya
lishe. Wananchi wanafika na kutoa kadi za kliniki za watoto kwa mhudumu wa
afya, na kisha huitwa jina kupatiwa huduma.
KILIO
CHA WANANCHI.
Uchunguzi umebaini kuwa kwa miaka kumi, wakazi wa eneo hilo
wamekuwa wakiomba kujengewa zahanati bila mafanikio.
Mkazi wa Mindu Lysia Kanuti anasema wamekuwa wanapewa ahadi
nyingi kutoka kwa viongozi bila mafanikio.
Anasema kuwa wamekuwa wakipata huduma chini ya mti, huku wakina
mama na watoto wanakaa chini, hali hii imekuwa ikijitokeza mara kwa mara lakini
ufumbuzi wa changamoto hiyo hauonekani.
Kanuti anasema wanapata huduma ya kliniki ya watoto chini ya
mti kutokana na kuishi umbali wa kilomita zaidi nane kutoka zahanati ilipo.
Anaiomba halmashauri,serikali kuu,na wadau wengine wa maendeleo
kuwasaidia ujenzi wa zahanati, ili kupunguza adha wanayoipata ya huduma ya
afya.
“Natumia usafiri wa pikipiki kutafuta huduma za afya,ni hatari
mama mjamzito kutumia usafiri wa pikipiki na baiskeli, si salama kwa afya ya
binadamu.”Anasema Salome.
Salome anasema wanashindwa kufanya shughuli za uzalishaji
kutokana na kutumia muda mwingi kutafuta huduma za afya, hivyo kujikuta wako
nyuma kimaendeleo.
Mkazi wa Mtaa wa Lugala katika Kata ya Mindu, Hawa Hamisi anasema
changamoto wanayopata katika vituo vya afya ni foleni kubwa inayotokana na
upungufu wa watoa huduma katika vituo vya afya, hususani vilivyopembezoni mwa
mji.
Hawa anasema usikivu wa watoa huduma umekuwa ukilalamikiwa sana,
lakini hakuna ufumbuzi wa tatizo hilo, wamekuwa wakitoa kauli chafu kwa
wagonjwa, tunaomba serikali ifuatilie na kuweza kutoa adhabu kwa
watakaobainika.
Pia anasema huduma ya mama na mtoto ipewe kipao mbele hususani
kwenye vituo na zahanati za kata ambako ndiko kwenye watu wengi wenye kuhitaji
kupatiwa huduma hiyo. Matibabu.
Anaongeza kuwa serikali ibadili utendaji wa utoaji wa huduma za
afya katika zahanati, ili siku za jumamosi na jumapili utoaji wa huduma uwepo.
Hiyo itasadia kupunguza foleni za wagonjwa siku za wiki.
WATAALAMU WA AFYA.
Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Madanganya, Theresia Kilua anasema
jengo la zahanati hiyo limepata ufa na uongozi wa halmashauri umewataka kutumia
nyumba ya watumishi kutoa huduma za afya.
Kilua anasema imepita miezi miwili toka kuhama kwenye jengo hilo
la kituo cha afya kilichojengwa kwa nguvu za wananchi kutokana na ubovu.
Anasema mazingira ya kazi ni magumu kutokana na jengo wanalotumia
hivi sasa kujengwa kwa mfumo wa nyumba ya kuishi na sio kwa kutolea
huduma za afya.
Kutokana na mazingira ya kata ya Mindu, anasema hulazimika
kupanga ratiba ya kutoa huduma ya vipimo, kliniki kwa watoto katika mitaa, na
huduma hiyo inajulikana huduma ya mkoba.
Pia anasema kuwa katika kutoa huduma ya mkoba kinachofanyika ni
vipimo kwa watoto, na kutoa ushauri kwa kina mama wajawazito,elimu ya lishe.
Anaongeza kuwa huduma ya mkoba inasaidia wananchi wanaoishi
mbali na vituo,kupunguza gharama za kusafiri kutafuta huduma ya Afya.
Chini ya utaratibu huo, wamekuwa wanatoa huduma kwa wananchi zaidi
ya 600 kwa siku. Huduma hiyo hufanyika mara moja kwa mwezi kwa mtaa.
Kwa upande mwingine anasema kuna baadhi ya wakina mama ni wavivu
kupeleka watoto kliniki, hata wao wenyewe kufika kupata vipimo na kwamba huduma
ya kuwafuata wananchi walioko mbali na vituo vya afya imewasaidia.
Theresia anasema kuwa changamoto kubwa katika zahanati ya
Madanganya ni ukosefu wa maji safi na salama. Wanatumia maji ya visima pia
hawana nishati ya umeme.
Mratibu wa huduma za Chanjo Manispaa ya Morogoro,Hidaya Omary
anasema wanalazimika kutoa huduma ya mkoba kutokana na ukosefu wa vituo vya
afya na zahanati karibu na wananchi.
Hidaya anasema watoa huduma ya mkoba katika maeneo ambayo hayana
zahanati wanapewa usafiri ili kuweza kuwafikia wananchi kwa wakati.
NINI
KIFANYIKE.
Huduma ya Afya inapaswa kuboreshwa na kufanyika katika jengo
maalumu lenye vigezo vinavyotakiwa, sio kufanyika chini ya mti na wananchi
kukaa chini, jambo ambalo sio salama kiafya.
Wahudumu wa Afya waongezwe katika vituo na zahanatiza
pembezoni,wapatiwe vyenzo muhimu ili kuweza kuwafikia wananchi popote walipo,
pia huduma ipatikane muda wote.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment