Diwani wa kata ya Mkuyuni wilaya ya Morogoro,Mwinyi Buyi akichangia mada katika mdahalo wa kujadili njia za kupunguza migogoro ya ardhi,ulioandaliwa na UMADEP kupitia PELUM-Tanzania. |
Mwamasishaji kutoka Chuo cha SUA,Emmanuel Malisa akionge na wananchi wa kijiji cha Mfumbwe kilichopo katika kata ya Mkuyuni wilaya ya Morogoro,jinsi ya kupunguza migogoro ya ardhi. |
WANANCHI wa Kijiji cha Luholole na Mfumbwe vilivyopo tarafa ya Mkuyuni Wilaya ya Morogoro, wameitupia lawama lawama ofisi ya Ardhi, mipango miji na vijiji Wilayani humo,wakidai imekuwa chanzo cha migogoro ya mipaka baina Kijiji kimoja na kingine.
Madai hayo yameibuka kijijini hapo katika katika mdahalo ulioandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Uluguru Mountains Agricultural Development Project (UMADEP) kupitia PELUM Tanzania,uliokuwa unajadili kuhusu nini kifanyike kumaliza migogoro ya ardhi vijijini.
Walisema kama hali itendelea hivyo na hatua za haraka hazitachukuliwa katika kuzuia migogoro ya mipaka baina a Luholole,Mfumbwe,Madami, inaweza kutokea migogoro mikubwa ya ardhi kwa makundi ya watu waliopo wilayani humo.
“Migogoro mingi ya ardhi mkoani Morogoro, imetokana na baadhi ya viongozi wa mkoa na wilaya, kuamua kuanzisha na kupima vijiji vipya bila kuhusisha viongozi wa vijiji husika, na matokeo yake kusababisha mvutano baina ya vijiji hivyo, na hata kupelekea uvunjifu wa amani.”alisema Shiwi Chalo kutoka kijiji cha Luholole.
Mkazi wa kijiji cha Mfumbwe ,Ashura Juma alisema kuwa wananchi wanailalamikia ofisi ya ardhi na watendaji wake kutokana na kuamua kufanya maamuzi ya kugawa vijiji wakiwa maofisini bila ya kuwashirikisha wananchi husika katika vijiji .
Alisema kuwa hali hii itaendelea kujitokeza katika wilaya ya Morogoro, kama ofisi ya ardhi haitabadili mfumo wa kutoa maamuzi bila kushirikisha wananchi kwenye vijiji husika.
Afisa mipango miji na vijiji wilaya ya Morogoro, Andrea Biashara alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo,na kuahidi kuzifanyia kazi na kuwataka wananachi wa vijiji husika kukaa meza moja na kukubaliana kabla ya wataalamu wa ardhi kushirikishwa.
Kwa upande wake Mhadhiri wa chuo kikuu cha kilimo( SUA), Emanuel Malisa aliwataka viongozi wa serikali ya vijiji , kushirikiana na kamati za usuluhishi ,mabaraza ya ardhi na watalaam wa ardhi katika kutatua migogoro yao ili kudumisha amani .
PELUM kwa kushirikiana na UMADEP wako katika utekelezaji wa mradi wa CEGO ambao unaendesha midahalo katika vijiji vya wilaya za Morogoro na Mvomero, midahalo ambayo ina lengo la kujadili namna nini kifanyike kupunguza migogoro ya ardhi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment