MAMA
wajawazito na wenye watoto wadogo katika kata ya Mindu Manispaa ya Morogoro
wamelzimika kupata huduma ya afya,chini ya mti kutokana na kukosekana huduma ya
kituo cha afya na zahanati kwa kipindi cha muda mrefu.
Kundi kubwa la kinamama wenye watoto wachanga kutoka ya mitaa nane ya kata ya Mindu wameonekana na wakipata
huduma za kliniki na chanjo chini ya mti katika ofisi ya kata hiyo.
Aidha akina mama hao walionekana wakiwa wamekaa chini ya miti kukiwa
hakuna benchi wala viti vya kusubiria huduma wakati wakiitwa mmoja mmoja kupata
huduma hiyo.
Mama Sharifa Duttilo alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakiomba
kujengewa Zahanati lakini hakuna juhudi zozote kutoka kwa viongozi wao zinazoonekana
kufanyika wala kuhamasisha wananchi kufanya ujenzi huo.
Sharifa anaiomba halmashauri,serikali kuu,na wadau wengine wa maendeleo
kuwasaidia ujenzi wa zahanati,kituo cha afya ili kupunguza adha wanayoipata ya
huduma ya afya kwa muda mrefu,ambayo wakati mwingine kukosa tiba za afya
kunaweza sababisha madhara makubwa zaidi.
Afisa mtendaji kata ya Mindu Laurent Masanja alisema tayari
wameunda kamati ya uhamasishaji kusaidia kukusanya michango mbalimbali kutoka
kwa wananchi na wadau wengine ili kukabiliana na changamoto hiyo ya zahanati.
Masanja alisema kamati hiyo imeundwa ili kuwataka wananchi
wenyewe kujitokeza, kuanza ujenzi kabla ya wadau wenguine kujitokeza,wakati
wakisubiri fedha kutoka halmashauri.
Diwani wa kata Mindu Hamis Msasa akisema changamoto hiyo imekuwa
ni ya muda mrefu lakini wamejitahidi kuweka mikakati ya kukabiliana na
changamoto ingawa kikwazo bado ni upatikanaji wa fedha za ujenzi.
Msasa alisema kwa kushirkiana na viongozi wa mitaa 8 husika
wanajipanga kumaliza kilio hicho cha afya, kwani hakuna kiongozi anapenda
wananchi wake wateseke,hivyo aliwataka wananchi kujitokeza kuchangia ujenzi wa
kituo cha afya pindi utakapoanza.
Kata ya mindu iliyopo Manispaa ya Mororogoro ina jumla ya wakazi
2384,shule za msingi 4,zahanati 1,hospitali 1 ya Mazimbu
No comments:
Post a Comment