Tuesday, September 13, 2016

RC.KEBWE,FEDHA ZA WATUMISHI HEWA ZIREJESHWE.

MKUU Wa mkoa Wa Morogoro Dk Steven Kebwe amezitaka halmashauri zote wilayani humo kuchukua hatua za haraka na kurudishwa fedha zilizochukuliwa na  watumishi hewa kwani muda uliotolewa wa kukamilisha zoezi hilo umeisha.

Dkt.Kebwe alitoa agizo hilo katika kikao cha siku mbili cha wajumbe wa ALAT mkoa Wa Morogoro kinachofanyika katika mji Wa Ifakara wilayani Kilombero.

Dk Kebwe alisema kuwa halmashauri za Wilaya katika mkoa huo zimekuwa kimya katika suala hilo kwani hadi hivi sasa ni Wilaya moja tu ya Kilosa ndio iliyofanyia kazi suala hilo na kufikisha taarifa yake katika ofisi ya Mkuu Wa mkoa.

Ameziagiza halmashauri zilizobaki kujitazama upya na  kuharakisha suala hilo kwani Fedha hizo zikirudishwa zitakwenda katika masuala mbalimbali ya wananchi ikiwemo kukamilisha madawati katika shule.

Alisema baada ya kuunda timu ya kujiridhisha ili kufuatilia idadi ya watumishi hewa mkoani humo ilibainika kuwa mkoa wa morogoro ulikuwa na watumishi  hewa 315 ambao wameitia hasara serikali kiasi cha shilingi bilioni 2.2.


Amebainisha kuwa hapo awali aliambiwa mkoa una watumishi hewa 149 tu na yeye kuamua kujiridhisha na baadae kubaini kuwa idadi aliyopewa mwanzo hata mara ya pili hazikuwa za kweli wowote.

Aidha Mkuu huyo amezitaka halmashauri hizo kusimamia na  kutenga fedha asilimia 10 zitakazokwenda kwa vikundi vya vijana na wanawake na  pia kujidhatiti na  kuhakikisha hakutokuwepo na  migogoro ya Ardhi katika halmashauri zao.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo Wa mkoa ameziagiza halmashauri hizo hadi mwisho wa mwezi huu ziwe zimepeleka mpango mkakati a kuongeza mapato katika halmashauri zao.


Awali akimkaribisha mkuu wa Mkoa,Mwenyekiti Wa Alat mkoa wa Morogoro Pascal Kihanga alisema lengo la kikao hicho cha siku mbili ni kufanya maandalizi kimkoa kwa ajili ya kikao cha Alat kitaifa kitakachofanyika Septemba 22 mwaka huu.

Kihanga alisema mafunzo hayo ni ya kuwajengea uwezo wajumbe tokana na  viongozi wapya kuwa wageni na pia kuelewa masual ya ulinzi na  Usalama na kujifunza mfumo Wa ukusanyaji wa mapato kieletroniki kama serikali kuu ilivyoagiza.


No comments:

Post a Comment