Friday, September 16, 2016

MWANAMKE ASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI KWA KUIBA MTOTO.

                             

JESHI  la Polisi Mkoani Morogoro linamshikilia mwanamke Anna Luambano  (33) mkazi wa Kipawa jijini Daressalam kwa kosa la kuiba mtoto mwenye umri wa siku 10 aliyefahamika kwa jina la Angel Meck mkazi wa Chamwino Manispaa ya Morogoro.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Ulrich Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba  13 majira ya asubuhi  ambapo askari polisi walipata taarifa za kuibiwa kwa mtoto huyo  kutoka kwa mama  wa mtoto huyo aliyefahamika kwa jina la Maimuna Mahmudu (20)  huko maeneo ya Kilimahewa.


Kamanda Mtei alisema kuwa  mtuhumiwa huo alikamatwa akiwa njiani maeneo ya Mdaula akiwa anelekea  Dar es salaam   anakoishi    mara baada ya kufanikiwa  kumdanganya   mama mzazi wa mtoto huyo  kutoka Hospitali ya Kata ya Mafisa  kuwa ampe ili  akamuonyeshe mume wake kuwa mtoto wa mdogo wake amejifungua  ili awape fedha za hongera kisha wagawane.


 Kamanda huyo alisema  kuwa mtuhumiwa  anahojiwa  na hatua za kumfikisha  mahakamani  zinafuata na kuwashukuru wale wote waliotoa ushirikiano hadi kufanikisha  kumkamata mwizi wa mtoto huyo    na kuwaomba kuendeleza ushirikiano na jeshi hilo ili kukomesha vitendo hivyo.


Kwa upande wake mtuhumiwa wa wizi wa Mtoto huyo aliwaambia wandishi wa habari kuwa alifanya kitendo hicho baada ya kutafuta kupata mtoto kwa muda mrefu bila mafanikio licha ya kuomba apewe  mtoto kutoka ustawi wa jamii ndipo akaamua kufanya kitendo hicho ili nae aweze kuwa na mtoto na kuitwa mama.


No comments:

Post a Comment