Thursday, April 17, 2014

TANESCO MOROGORO LAWAMANI



WANANCHI wa tarafa ya  Mang’ula Wilayani Kilombero mkoani Morogoro wamelitupia lawama shirika la umeme nchini (TANESCO),kutorekebisha miundombinu yake katika eneo hilo, na kusababisha kifo cha mtoto Amon  Ndawala mwenye umri wa miaka mitano


Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi katika kijiji cha Mang’la,walisema kuwa kifo cha mtoto huyo kilisababishwa na kupigwa shoti ya umeme, baadaya kugusana na nyaya za umeme zinazoshikilia nguzo ambazo ziko mbele ya nyumba ya fundi washirika hilo, ambazo kikawaida hazipaswi kuwa na umeme.

 Wananchi hao walilalamikia hatari ya miundo mbinu ya umeme katika eneo hilo, ikiwemo nyaya za shirika hilo kugusa juu ya paa za baadhi ya nyumba za watu  huku nyingine zikigusana na miti ama  kuning’inia njiani, jambo walilodai kuzidi kuwatia hofu na kutia maisha ya wananchi hao katika mazingira ya hatari.

Walidai kuwa kifo cha mtoto huyo kilitokea wakati alipokuwa akicheza  na watoto wenzake ndipo alipogusa waya unaoshikilia nguzo ya umeme na kunaswa katika nguzo hiyo ndipo watoto wenzake walipoenda kutoa taarifa kwamba mwenzao ameanguka na kushindwa kuinuka katika eneo.


Walisema kuwa wamekuwa wakitoa taarifa za mara kwa mara kwa viongozi wa shirika hilo kuhusiana na mazingira ya hatari ya Miundo mbinu ya Tanesco, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kurekebisha.

Juhudi za kuwapata wasemaji wa shirika la umeme zilishindikana na baada ya kuelezwa Meneja aliyekuwepo amehama kikazi mkoa, huku mtu mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Ester akidaiwa ndiye msemaji, naye akiwa kikazi nje ya Mkoa, ambapo simu yake ilipopigwa hakupokea kwa mara kadhaa na wakati mwingine kuonekana imezimwa.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro John Laswai, aliahidi kufanyia kazi changamoto za uchelewaji wa askari wanaoitwa na kuchelewa kufika katika matukio ya dharura, kama ilivyolalamikiwa na wananchi, huku akikiri kifo cha mtoto huyo, na kwamba bado polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi wa tukio hilo.

Mwisho

No comments:

Post a Comment