Mmoja wa mkazi wa Kilosa aliyeruhiwa kutokana na mgogoro wa ardhi. |
Morogoro ina eneo la kilomita za mraba
73,039,na eneo la hekta 2,226,396 za ardhi zifaazo kwa kilimo sawa na
asilimia 30.43 ya ardhi yenye rutuba inayofaa kwa uzalishaji
Mkoa una mashamba pori 220 ya vigogo ambayo hayaendelezwi na serikali ikishindwa kuchukua hatua za haraka kulipatia ufumbuzi suala hilo huku wananchi wakiwa wanalumbana kuhusu mashamba hayo
Mapori hayo yamekuwa chanzo cha kuzuka kwa migogoro na kikwanzo cha utekelezaji wa agizo la rais la kuufanya mkoa huo kuwa ghala la taifa la chakula jambo ambalo mpaka sasa limeshindwa kutekelezeka
Rais Jakaya Kikwete alipofanya ziara mkoani Mororo alitoa agizo hilo la mkoa huo kuufanya kuwa ghala la chakula akiamini kuwa una ardhi na rutuba ya kutosha kuzalisha chakula cha kukidhi mahitaji ya mkoa na nchi.
Morogoro iliingizwa kwenye kundi la mikoa sita inayozalisha chakula kwa wingi nchini,Mgawanyo mpya wa mikoa uliofanywa hivi karibuni umechangia ongezeko la mikoa hiyo hadi kufikia mikoa saba.
Mikoa hiyo ni Mbeya, Ruvuma, Rukwa, Njombe, Katavi, Iringa, Kigoma na Morogoro,na kufikia lengo hilo, Morogoro iliweka mpango maalum ujulikanao kama Fanya Morogoro kuwa Ghala la Taifa la Chakula (Famogata).
Hata hivyo, mpango huo umeshindwa kufanikiwa kutokana na changamoto nyingi ikiwemo ardhi kubwa kumilikiwa na vigogo wengi wa ndani ya mkoa na nje ya morogoro wanaoshindwa kuiendeleza maeneo yao ambayo yanatakiwa katika uzalishaji
Kaimu Katibu tawala (Uchumi na fedha) mkoa wa Morogoro, Lamiki Noah, aliwaambia wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi iliyotembelea mkoa huo wa Morogoro kuwa mashamba ya vigogo ambayo pia yanajulikana kuwa ni mashamba pori yaliyoachwa bila kuendelezwa kwa miaka mingi yamekuwa kikwazo cha utekelezaji wa Famogata.
Kutokana na eneo kubwa la ardhi hiyo kuchukuliwa na wawezekezaji na vigogo serikalini, kupanuka kwa makazi ya watu na ogezeko la kasi la idadi ya mifugo kumesababisha migogoro mingi kutokana na uhaba wa ardhi.
Mkoa wa Morogoro una zaidi ya ng’ombe 1,222,373 na inaongezeaka kila mwaka . Wataalam wanasema kuwa ng’ombe mmoja anahitaji ekari moja na robo kwa ajili ya malisho yake kwa mwaka.
Hivyo mahitaji makubwa ya ardhi ya malisho ya mifugo, kilimo na makazi kumekuwa kunaibuka migogoro mingi hasa baina ya wakulima na wafugaji kwa upande mmoja na wananchi na wawekezaji kwa upande mwingine.
Migogoro hiyo imeshamiri zaidi katika wilaya za Kilosa, Kilombero, Mvomero, Morogoro na Ulanga. Wakulima na wafugaji hugombea ardhi ndogo iliyopo na nyingine ikimilikwa na vigogo na wawekezaji
Kuwepo kwa mashamba pori zaidi ya 220 ya vigogo umekuwa ukizua vurugu kwa sababu wananchi wengi hukosa ardhi kwa ajili ya kilimo hulazimika kuyavamia mashamba hayo yaliyodumu kwa muda mrefu bila kuendelezwa ili yatumike kuzalisha chakula kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao.
Katika siku za hivi karibuni kaya zaidi ya 50 za wakazi wa kitongoji cha Mateteni kata ya Mbigiri wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro walijikuta wakipata hifadhi kwenye mahema baada ya nyumba zao kuvunjwa kwa tingatinga na watu waliodai kuwa ni madalali wa mahakama waliotumwa na aliyekuwa katibu mkuu kiongozi wa utawala wa awamu ya kwanza, Thimos Apio.
Tukio hilo lilikuja baada ya familia hizo awali kukumbwa na mafuriko na uongozi wa mkoa wa Morogoro kuamua wahamishiwe katika eneo la mwinuko lilipo shamba la ( Apiyo) ili kujistiri kwa muda wakati serikali ikifanya jitihada za kuwatafutia eneo jingine la kudumu.
Uvunjaji huo usiozingatia utu umesababisha familia kuishi kwenye mahema yaliyotolewa na aliye kuwa mkuu wa wilaya hiyo, Halima Dendego, baada ya kupata taarifa za tukio hilo.
Mahema hayo yanayotoa hifadhi dhidi ya mvua na jua, lakini hayana staha kwa sababu baadhi ya familia zinalazimika kuishi katika hema moja pasipo kujali jinsi na mahusiano yao.
Tofauti na mwekezaji Apiyo,wapo viongozi wengi wanaotajwa kumiliki mashamba makubwa mkoani Morogoro wakiwemo, marais wastaafu , Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, Fredrick Sumaye na John Malecela, mawaziri, wabunge na baadhi ya viongozi wa serikali.
Mashamba yanayomilikiwa na vigogo hao yametajwa kuchangia migogoro ya ardhi isiyoisha katika mkoa wa Morogoro, kwa kuwa idadi kubwa ya wananchi hawana maeneo ya kulima hali inayowalazimu kuyavamia mashamba ya vigogo yaliyotelekezwa.
Mkoa baada ya kubaini kiini cha migogoro mingi ya ardhi uliamua kubainisha mashamba yote yasiyoendelezwa yaliyobakia kama mashamba pori kwa muda mrefu ili kumwomba rais mwenye dhamana ya ardhi kwa mujibu wa sheria kubadilisha matumizi ya mashamba hayo.
Hata hivyo, Rais Jakaya Kikwete wakati akizungumza na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam alisisitiza kuwa hatakuwa tayari kubadilisha matumizi ya ardhi yoyote iliyomilikiwa kihalali hadi atakapopewa sababu za kuridhisha za kubadilisha matumizi hayo.
Saidi Mkwida mkulima kutoka Wilaya ya Kilosa anasema kuwa tatizo la migogoro ya ardhi katika mkoa wa Morogoro umekuwa sugu na kila Mkuu wa mkoa anayehamishiwa mkoani hapo anaikuta na hatimaye anahamishwa bila kupatiwa ufumbuzi wowote jambo ambalo linatia shaka huku wananchi wakiendelea kulumbana
Mkwida anasema tatizo kubwa swala hilo linaendeshwa
kisiasa sana na kutokana na maagizo mengi yanatolewa na viongozi wa juu wa
serikali hayafanyiwi utekelezaji na hivyo wananchi wakibaki wakisubiri suluhu
kila mwaka bila mafanikio yoyote
Anasema kuwa kinachotakiwa kufanyika maeneo yote
yenye migogoro yafanyiwe uchunguzi kwa kina kujua tatizo nini ili kuweza
kupatiwa ufumbuzi wa kudumu,na serikali kufuatilia mapori yote yanayomilikiwa
na vigogo na kutoendelezwa yajulikane na kuweza kupewa wananchi wanaopigania
ardhi ya kulima na kufuga
Peter Kimath
No comments:
Post a Comment