Tuesday, December 11, 2012

DC,WAFUGAJI ACHENI KUTOA RUSHWA KWA VIONGOZI WA SERIKALI

SERIKALI wilayani Mvomero imewataka wafugaji kuacha kugeuka mitaji ya baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali, kwa kuwahonga fedha kwaajili ya kuwalinda pindi wanapokwaruzana na wakulima, au kuvunja sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

Mkuu wa wilaya ya Mvomero Anthony Mtaka, alisema hayo wakati akiongea na kikundi cha wafugaji kinachokutana mjini Morogoro kujadili na kuweka mikakati ya namna ya kufikia maendeleo kwa jamii hiyo.

Alisema wakati mwingine wafugaji huendekeza migogoro kwa kutoa rushwa ili walindwe, jambo ambalo mwisho wa siku ni lazima sheria ifuate mkondo wake na viongozi wanaobainika kuwajibishwa ama kufukuzwa madarakani.

Aliwasisitiza wafugaji  kuzingatia kupunguza mifugo, kufuga kisasa na kutowaruhusu wafugaji wageni kuingia katika maeneo yao kwani wao ndio ambao wamekuwa wakichangia migogoro katika maeneo yao kwa mifugo kuonekana kuzidi.

Wafugaji ni watanzania kama walivyo watanzania wengine, kutatua mgogoro wa wafugaji hakumaanishi unatatua mgogoro kati ya watanzania na raia wengine wa kigeni, hivyo naamini matatizo na changamoto zenu mnaweza kuzijadili na kuzitatua katika vikao husika, mfugaji kulisha kwenye shamba la mkulima unajua ni kumpa mkulima hasara kubwa ikizingatiwa mtaji wake katika kilimo ni mdogo, tofauti na wewe ukiuza ng’ombe mmoja, unamudu maisha, lakini kikubwa ni wafugaji mnaowakaribisha kutoka maeneo mengine”Alisisitiza Mtaka.

Aidha mkuu huyo wa Wilaya,alisema umri sio kigezo cha kumfanya mtu kuwa kiongozi,badala yake uongozi ni utashi wa utayari wa kujifunza katika mazingira na namna ya kupata majawabu ya changamoto zilizopo.

Alisema hata mchakato wa mageuzi unaoendelea katika nchi mbalimbali duniani hautokani na kuwataa kutokana umri walio nao viongozi walio madarakani, bali ni utashi wao na mahitaji katika uongozi wao.

Alibainisha hayo ikiwa ni siku chache tantu baadhi ya viongozi mbalimbali wa kisiasa kupitia mdahalo ulioendeshwa Chuo kikuu, kutaka Raisi ajaye awe ni aliyezaliwa kuanzia mwaka 1961  na kuendelea na sio kabla ya hapo,  ambapo alisema  umri upo wa aina mbili ukiwemo wa vijana wenye fikra za kizee na wazee wenye fikra za ujana, na wapo vijana na hata wazee waliopewa madaraka na kufanya ovyo, vivyo hivyo wapo waliofanya vizuri kwa pande zote mbili.

Naye mmoja wa wafugaji, aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa wa Morogoro na mikoa mingine, Stephen Mashishanga,aliwaasa wafugaji kuzingatia sheria katika utendaji wa mambo yao.

Kiongozi wa jamii ya wafugaji wa kimasai,Laigwanan Sawasawa Lopejo alidai Serikali itaweza kudhibiti uingiaji holela wa mifugo iwapo viongozi wake watawadhibiti wafugaji hao wageni wanaopita katika maeneo yao ambao wameendelea kuingia makundi kwa makundi na kuacha kule walikopangiwa kuelekea.

Akizungumzia kikao hicho, mratibu toka taasisi ya PAICODECO inayohusika na maendeleo ya wafugaji, Mwarabu Ole Paulo, alisema bado jamii hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali hasa katika sekta ya elimu na ardhi, na kwamba mabadiliko ya tabia nchi yaliyosababisha ukame yamewaathiri wafugaji wengi ambao wamepoteza mifugo yao.

No comments:

Post a Comment