Na,Peter Kimath.
AZIMIO la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu,
linaamini kwamba binadamu wote ni sawa, licha ya kuishi katika mazingira
tofauti.
Hali tofauti za maisha na kutokubaguana kwa dini,
rangi hata kabila ndiyo ubinadamu wenyewe.
Pamoja na kuwepo kwa misingi ya ubinadamu, bado
jami ya watu wenye ulemavu wamekuwa wakitengwa nchini Tanzania na kukosa huduma
muhimu.
Vitendo vya kuwaficha watoto wenye ulemavu ndani
vimetapakaa katika maeneo mengi ya nchi. Si Mvomero pekee.
Kilio hicho kimekuwa kinapigiwa kelele na
wadau mbalimbali, bila mafanikio yoyote.
Serikali kwa upande wake imekuwa ikifumba macho
na masikio, bila kuweka mkakati wowote wa kumaliza janga hilo.
Mashirika yasiyo ya kiserikali na taasisi za dini
ni miongoni mwa wadau ambao wamekuwa wakiisaidia serikali kuchochea maendeleo,
ikiwemo kupiga vita ya ubaguzi, kutetea haki za wenye ulemavu waliopo ndani ya
jamii.
Mkurugenzi wa Kituo cha Wasaidizi wa Kisheria Morogoro(MPLC),Flora
Masoyi anasema kuwa wamekuwa wakitetea haki za watoto wote bila ubaguzi wowote
pale wanapoletewa kesi, taasisi yao inatoa msaada wa kisheria hivyo ni mara
chache sana wanapokea kesi za wenye ulemavu.
Masoy anasema katika kuhakikisha jamii inapata huduma
sahihi, ndani ya mkoa wa Morogoro wamefungua kituo kila wilaya, lengo likiwa ni
kusogeza huduma karibu na wananchi, hata wasiojiweza kuweza kufika na kupatiwa
msaada.
Anasema kuwa wamekuwa wakitoa elimu kwa makundi mbalimbali,
wakiwemo wasaidizi wa kisheria kila kijiji, wananchi, lengo likiwa ni kutoa
elimu juu ya ukatili unaofanyika ndani ya jamii, ikiwemo sakata la kuwaficha
wenye ulemavu ndani.
Anasema katika kufanikisha zoezi la utoaji wa elimu, wanashirikisha
viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya wilaya hadi vitongoji,hushirikishwaji
wanaofanya umewasaida kwa kiasi kikubwa elimu kusambaa na kuweza kupunguza
ukatili ndani ya jamii.
Anasema ili kufanikisha janga la wenye ulemavu kufichwa ndani
katika baadhi ya vijiji wilayani Mvomero, taasisi ziache kukaa mijini na kwenda
kuweka kambi vijijini, kwani utakuta ofisi ya taasisi/asasi iko mjini wakati
walengwa wake wapo vijijini.
Pia anasema taasisi/asasi kutokuwa karibu na wananchi ni sababu
ambayo inazifanya familia zenye watoto wenye ulemavu kuwaficha ndani, hivyo
kukosa msaada wa elimu ya matunzo ya wenye ulemavu.
Pia anasema kuwa taasisi binafsi/mashirika, serikali zijikite
maeneo ya vijijini kutoa elimu kwa wananchi, kujua haki za watoto, haki za
binadamu, haki za wenye ulemavu.
Kwa kufanya hivyo, kutasaidia kupunguza janga la kuficha
watoto wenye ulemavu ndani.
Mshauri wa Taasisi ya Eric Memorial Foundation iliyopo Wilayani
Mvomero,Josephine Bakita anasema changamoto kubwa iliyopo katika jamii, ni
kukosa hamasa kuhusu haki za wenye ulemavu na kwamba hata wazazi wenyewe,
huchangia ubaguzi kwa kundi hili.
Taasisi hiyo ambayo ndiyo pekee iliyopo Mvomero inayosadia
kundi la wenye ulemavu, ilihamishia ofisi zake katika kata ya Mvomero kutokana
na idadi kubwa ya watoto wenye uelemavu, ambapo wazazina walezi wanahitaji
kupatiwa elimu ya jinsi ya kuishi na kundi hilo.
Bakita anasema kuwa wamekuwa wakifanya kazi kwa kushirikiana
na serikali ya wilaya, kata, kijiji, pamoja na kitongoji.
Mfumo huo wa kazi shirikishi umekuwa ukiwasaidia sana kujua pale
watoto walipo na kuweza kutoa elimu kwa walezi wa watoto hao.
“Tunatembea kwa miguu nyumba kwa nyumba katika vijiji vya
Mvomero kuwatambua watoto wenye ulemavu waliofichwa ndani. Familia nyingine
hazitaki watoto wao watambulike,”anasema.
Anasema kuwa wamekuwa wakifanya semina katika vijiji vya Mvomero
kuhusu elimu ya malezi ya watoto wenye ulemavu, kujua haki za watoto, na jinsi
ya kutoa taarifa pindi wanapoona mtoto mwenye ulemavu amefichwa ndani ili aweze
kusaidiwa.
“Siku moja katika safari zangu nikaona kwa mbali kama vile
familia imefuga tumbili na kafungwa kwa kamba kwenye mti wa Mwembe,
nilivyokaribia nikaona kumbe ni binadamu. Nikafika nyumbani pale na kumfungua
mtoto huyo, aliyeitwa Silus,”anasema Josephine.
Pia anasema ili kuokoa kundi la wenye ulemavu wa akili na viungo
taasisi zinapaswa kuwa karibu na kundi la wenye ulemavu. Watendaji kwa upande
wao sharti wapate mafunzo ya kuhudumia kundi hilo.
Kwa kufanya hivyo, anasema wataondokana na unyanyapaa na
kuyafahamu makundi yote ya wenye walemavu.
Anaongeza kuwa matukio ya kikatili ya kutisha kwa wenye
ulemavu hapa nchini yanatokana na uelewa finyu kuhusu haki za wenye ulemavu,
hivyo wengi wanaona mlemavu hana haki ya kuishi wala kupata huduma za
afya.
Anasema kama ambavyo serikali ilivyostuka kwa watu wenye
ualbino, inapaswa sasa kuchukua hatua kwa wote wasiojiweza na maisha yao
siku zote kuishia kulala kitandani.
Ameomba ianzishwe kampeni katika kila kijiji, kitongoji, kata na
wilaya kuchambua makundi yote ya wenye ulemavu na kila kundi litetewe kwa uzito
wake.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ndole, kata ya Kinda,Wilaya ya Mvomero,
Andrian Lucas anasema kuwa uwepo taasisi binafsi umewasadia wenye ulemavu
katika maeneo ya vijijini, hususan katika kuchochoea maendeleo
kutokana na serikali kusahau wananchi wa chini.
Lucas anasema familia zenye watoto wenye ulemavu nyingi
zimegundulika baada ya taasisi binafsi kuingia kijijini hapo na kutoa elimu juu
ya wenye ulemavu, na namna ya kuwatunza, kwani wengi wao walikuwa
wanafungiwa ndani kama wanyama.
“Tunashukuru taasisis ya Eric Memorial Foundation kwa kufika
kijijini kwetu, hii imesadia kugundua watoto wenye ulemavu waliofichwa ndani.
Hivyo naomba serikali kushirikiana na taasisi hii katika kuwatetea walemavu
waliofichwa ndani,” anasema.
Anasema kuwa kutokana na serikali ya kijiji kutokuwa na ratiba
wala bajeti ya kufanya sensa ya wenye ulemavu, huwa wanafanyakazi kwa
kushirikiana na taasisi binafsi, pindi wanapofika kutembelea familia zenye
walemavu.
Kwa upande mwingine, anaomba serikali kuanzai ngazi ya
wilaya hadi mkoa, kutuma wataalamu wa afya kutembea maeneo ya vijijini, ili
waweze kuwatambua wenye ulemavu,kujua idadi yao na kuwapatia msaada,
badala ya kazi hiyo kuziachia taasisi binafsi pekee.
Naye Mkazi wa Makuyu, Catherine Antony anasema uwepo wa taasisi
binafsi zinazosaidia wenye ulemavu, zimewafumbua macho na kutambua kuwa
kujifungua mlemavu si mkosi wala kulogwa, na kwamba watoto hao wanatakiwa
kupata haki zote kama watoto wasio na ulemavu.
“Katika kijiji chetu hivi sasa mama akijifungua mtoto mwenye
ulemavu, anajitokeza ndani ya jamii, anatoa taarifa kwa viongozi wa kijiji, kwa
taasisi binafsi, hakuna familia inaficha tena mtoto ndani kutokana na elimu
iliyosambazwa,” anasema.
Catherine anasema umefika wakati asasi zipewe ushirikiano pindi
zinapofika maeneo ya vijijini kufanya kazi ya kuchochea maendeleo.
Pia amewaomba viongozi wa vijiji kuwa bega kwa bega na asasi
hizo, kutokana utendaji wao kuwa na tija katika jamii.
Anasema kutokana na idadi ya watoto wenye ulemavu waliopo katika
Wilaya hiyo, bado kuna haja ya asasi/mashirika kujitokeza kuzisadia familia
zenye watoto hao, kujenga kituo cha kuwalea na kuweza kupata huduma ya elimu
kulingana na aina ya ulemavu uliopo.
Katika wilaya ya Mvomero kuna watu wenye ulemavu zaidi ya 200,
wanahitaji huduma sawa kama binadamu wengine wasio walemavu.
Naye Mkurugenzi wa Asasi ya Young Strong Mothers Foundation (YSMF)
Jackiline Bomboma anasema taasisi ambazo zimejisajili kufanya kazi za kusaidia
wenye ulemavu zifanye kazi kwa mujibu wa sheria ili kuisadia serikali katika
sekta hii, kutokana na serikali kutokuwa na wataalamu wa kutosha kutembea kila
kijiji.
Bomboma anasema mashirika na taasisi binafsi zinapaswa kuungana na
serikali katika kupambana na sakata la watoto wenye ulemavu kufichwa ndani,
kutoa elimu, na kila wanapokutana na wananchi wazungumzie janga hilo kama
ilivyo janga la ugonjwa ukimwi, ambao unapigwa vita.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment