MKUU wa wilaya ya Morogoro Said Amanzi, amewataka watendaji vijiji na kata kutokuwa chanzo cha migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji ambayo inatokea kila wakati katika wilaya hiyo kutokana na wafugaji kupewa maeneo bila kufuata sheria
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake,alisema kuwa migogoro hiyo imekuwa ikisababishwa na baadhi ya watendaji kutoa vibali vya maeneo kwa baadhi ya wafugaji na hivyo kuwapo kwa migogoro isiyo malizika katika maeneo ya kijiji cha Bonye tarafa ya Bwakila.
Amanzi alisema kuwa wilaya ya Morogoro ni moja ya wilaya inayoingiliwa na kuvamiwa na wafugaji kutoka katika mikoa ya Mbeya,Iringa na ile ya kanda ya ziwa lakini kuvamiwa huko kunatokana na baadhi ya watendaji kuanzia ngazi ya vitongoji,vijiji na kata kuwatokuwa waaminifu kwa kuwaingiza kiholela.
Aliwataka wananchi waliopo maeneo yanayovamiwa kutoa taarifa kwake badala ya kujichukulia hatua mikononi na hivyo kuwapo kwa migongano isiyokuwa na msingi na kusitisha shughuli za maendeleo katika maeneo yao.
Hata hivyo alisema kuwa ni vyema watendaji wakashirikiana na wananchi katika baadhi ya maamuzi kwa kuitisha mikutano mikuu ya vijiji ili kuondokana na migogoro ambayo imekuwa ikitokea kila wakati na kusababisha uvunjifu wa amani na upotevu wa mali.
mwisho..
No comments:
Post a Comment