Friday, August 21, 2015

WANAWAKE MATOMBO WALIA NA RUSHWA KATIKA UCHAGUZI

WANANWAKE katika Wilaya ya Morogoro Tarafa ya Matombo mkoani Morogoro wamesema rushwa ndio inachangia kwa kiasi kikubwa kushindwa kushiriki katika chaguzi mbalimbali zinazofanyika kila nchini kutokana na hali zao za uchumi kuwa duni


Hayo yalisemwa katika mdahalo wa Wanawake na Uchaguzi ulioandaliwa na Kituo cha Msaada wa Wasaidizi wa Kisheria (MPLC) kwa ufadhili wa OXFAM Tanzania katika program ya Fahamu Ongea sikilizwa iliyoshirikisha wanawake kutoka kata za Konde,Mkuyuni,Kiloka,Mkamba na Kisemo katika Tarafa ya Matombo

Geniveva Peter na Zuhura Mfalme walisema kuwa katika kipindi cha uchaguzi rushwa inatawala hasa ukikuta mwanamke ni miongoni mwa wagombea anajikuta anashindwa siku zote kutokana na mpinzani wake kuwa na kipato cha juu na kuweza kuwapa wapiga kura ili wampatie ushindi

“viongozi hivi sasa kwa asilimia kubwa wanapatikana kwa kutoa rushwa,hivyo wanawake tunapaswa kubadilika na kufanya maamuzi ya kuwachagua viongozi bora na sio wanaotokana na rushwa za fedha na vitenge ambao wakipata uongozi wanajali maslahi yao”Walisema

Kwa upande wake Afisa wa Haki na Jinsia  kutoka OXFARM Tanzania,Rashida Shariff alisema katika program ya Fahamu Ongea Sikilizwa lengo lake ni kuhamasisha wanawake  na vijana kushiriki katika uchaguzi mkuu,na kupatiwa elimu ya uchaguzi huru na haki ili kuweza kupata fursa ya kutambua kiongozi gani anafaa kuongozi jamii

Rashida alisema wanawake wamekuwa wakidhalilishwa sana kipindi cha uchaguzi kwa matusi,na kashfa na wamekuwa wakitumiwa sana kama madaraja ya rushwa na wagombea na kujisahau kama wao ni waathirika wakubwa pindi watakapomchagua kiongozi ambaye hatawajali na kujali maslahi binafsi

Aliwataka wanawake wasikubali kuwa watumwa wa rushwa katika kipindi cha uchaguzi,kutokubali kushurutishwa na wanaume kupiga kura kwa kiongozi ambaye hampendi,na kutunza vitambulisho vya kupiga kura ili visije kuibiwa na kufichwa na wapenzi wao ama marafiki wenye kumpenda mgombea fulani kwa maslahi binafsi

Mkurugenzi wa Kituo cha Msaada wa Wasaidizi wa Kisheria,Flora Masoyi,aliwataka wanawake kutambua kuwa kura ni siri,pia kutambua matatizo ya wanawake ni mengi na hayana chama,hivyo ni wakati wa kuchagua kiongozi bora ambaye ataweza kupambana na changamoto zinazowakabili wanawake nchini

Mwisho.


No comments:

Post a Comment