KATIKA hali inayoonesha ni kuendeleza mapambano na msuguano wa mimi nani, polisi jana ilizuia maandamano ya wandishi wa habari mkoani Dodoma yalipangwa kufanyika 11.9.2012 katika nchi nzima kulaani kitendo cha Jeshi hilo kumuua kinyama mwandishi mwenzao Daudi Mwangosi wa Channel Ten alipigwa na Bomu na mwili wake kusalia vipande vipande Septemba 2 mwaka huu Nyololo Iringa.
Haiingii akilini Jeshi hilo linafanya hivyo kuunga Mkono kilichofanywa na wenzao kule Nyololo Iringa kuwa ni halali au wanafanya hivyo kuenzi maamuzi yaliyotekelezwa na uongozi wa Polisi kwamba ni wa haki, au linafanya hivyo ili kuonesha kuwa hizi ni zama za nguvu ya Polisi.
Wakati wananchi nchi nzima bado wana maumivu ya tukio hilo na hivyo kutaka kupaza sauti kwamba kitendo kilichofanywa si sahihi, bado Polisi jana mkoani Dodoma kupitia kwa OCD wa Wilaya ya Dodoma mjini jina linahifadhiwa, aliendeleza kile kinachoonekana kukomoana baada ya kukwamisha maandamano ya wandishi wa mkoani humo, kwa madai walichelewa kupeleka taarifa na hivyo kukiuka muda wa masaa 48.
Yawezekana ni kweli Uongozi wa wandishi unaweza ukawa umekosea lakini katika maombolezi yaliyo sasa nchini na kauli mbali zilizotolewa kuhusu kifo cha Mwangosi, haikuwa busara kwa kiongozi yeyote kukataa kile kinachoombwa na wandishi hao, kilichotakiwa kitumike ni busara na utu ili tendo hilo lifanyike ili kutoa hisia za kwamba pengine polisi Dodoma inaunga mkono au kukubaliana na kifo cha marehemu Mwangosi, na kma halikubaliani, lingetowa kibali badala ya kuzuia.
Kutokana na kitendo hicho kilichofanywa na polisi, wadau mbalimbali mkoani Dodoma, wamekuwa na maoni mbalimbali ambapo, wengi wao wanasema, Polisi Dodoma imekuwa na hasira kwa kile kilichoelezwa baadhi ya Askari waliohusika katika mauaji na zoezi zima la Nyololo, walikuwa wametoka Dodoma na Morogoro.
Baadhi yao waliotoa michango wakati wa kukusanya dodoso za makala hii walisema, huenda polisi Dodoma nao wamewanyima wandishi kibali kwa sababu wanomboleza kwa mwenzao kujeruhiwa mguuni, lakini wanadai isingekuwa sababu yenye mashiko ya kupelekea kuwanyima kibali hicho.
Katika mila na desturi mbalimbali nchini, huwa watu wanotuhumiwa uchawi miongoni mwa koo, na kama kikitokea kifo chochote kilichosababishwa na mmoja wa ndugu au anayebashiriwa kuwa ndiye mchawi, kwa mintarafu kujificha asioneka kuwa yeye ndiye mhusika, hata siku moja huwa hakosi kwenye msiba au kilio hicho.
Kwa mila hizo za jadi, mchawi au mtuhumiwa na kifo miongoni jamii hiyo, huwa wa kwanza hata kutoa sanda na gharama za maziko, na wakati mwingine huwa analia kuliko watu wengine ili kujificha asitafsiriwe kuwa yeye ndiye amesababisha mauaji hayo..
Lakini nashangaa Jeshi la Poisi Dodoma halikuwa kama watu wa jadi ya kwetu ambao huwa wanajificha kwenye pazia ya kujishughulisha kwenye msiba na kutoa sanda na kulia kwa nguvu kuliko watu wengine, lakini wao wamethubutu kuendelea kukataa kuwanyima wandishi wa Dodoma kibali cha kuandamano kwa zisizo pevu.
Aidha pamoja na kwamba wale waganga wa jadi kwetu wanaotuhumiwa kuhusika na kifo cha msiba ndani ukoo huwa wanakuwa wa kwanza hata kufika kwenye matanga, Polisi wa Dodoma wameshindwa kufanya hivyo, na badala yake wameonesha ulimbwende wa kazi yao kiasi cha kuwanyima hata kuomboleza na kushiriki matanga.
Hata hivyo ninachofahamu kule kwetu, wahusika tukio la msiba, huwa wanakuwa wa kwanza hata kunawa na kula chakula cha msiba huo, na kwa kujibaraguza huwa mara chache kuondoka kwenye msiba huo kama watu wengine, agharabu huwa wanajitahidi wawepo hadi washiriki kuoasha vyombo vya chakula kwa wanawake, na kwa upande wa wanume hadi kukunja majamvi na kubomoa hema.
Kama nilivyosema hapo nyuma, Polisi Dodoma wameshindwa kujificha kwenye pazia hilo, maana kwa kutoa kibali cha maandano kwa wandishi hao ingeonesha jinsi walivyo makini na weledi kwa kujali mustakabali mzima wa tatizo lililotokea na kuondoa hisia zote machoni mwa watu.
No comments:
Post a Comment