WANASHERIA nchini wametakiwa kutumia
elimu waliyo nayo katika kuelimisha
jamii iishiyo vijijini kutokana na kuwa na uelewa mdogo katika kujua mambo mbalimbali ya kisheria ikiwemo kujua sheria na haki zao.
Mwito huo umetolewa na Mwanasheria Mshauri, Mtafiti na Mtetezi wa
Haki za Binadamu Mkoani Morogoro,Amani Mwaipaja ,ambapo alisema kuwa utambuzi
wa sheria umekuwa changamoto kubwa sana katika maeneo ya vijijini
Mwaipaja alisema kuwa wasomi wengi wamekuwa wakikimbilia mjini
wakiamini kuwa ndiko kwenye maslahi zaidi lakini wanasahau kuwa kujitolea
kusaidia jamii ni sehemu ya kujiajiri kwa kuwa jamii kubwa hasa ya maeneoo ya
vijijini inakabiliwa na changamoto nyingi za kisheria.
Alisema kuwa changamoto hizo ni pamoja na migogoro ya ardhi, masuala ya ndoa na talaka,
migogoro ya mirathi
pamoja na ugumu wa upatikanaji wa huduma za kisheria ambapo wananchi wengi
hulazimika kutembea umbali mrefu kuitafuta huduma hiyo.
“Nawaomba wasomi wa sheria mtumie
muda wenu katika kubuni njia rahisi ya kusambaza elimu ya sheria katika maeneo
ya vijijini kwa kutumia vyombo vya habari
kwani vina nafasi kubwa sana katika jamii”alisema Mwaipaja.
Aliwataka wasomi kuandika vitabu vya
sheria kwa lugha ya kiswahili pamoja na kutayarisha vipeperushi na
vijarida vitakavyomsaidia mwananchi wa kawaida kuelewa haki zake na
kuzifuatilia
Katika kuonyesha mfano kwa wasomi,
Mwanasheria Mwaipaja ametoa kitabu cha Zijue Sheria na Haki Zako, ambacho
kinaelezea kuhusu shera na taratibu mbalimbali anazopaswa kuzifuata mwananchi
ili aweze kupata haki zake. kitabu cha Zijue Sheria na Haki Zako tayari
kimeanza kusambazwa katika wilaya zote za Mkoa wa Morogoro.
Mwisho
No comments:
Post a Comment