KAYA zaidi ya 270 zikiwemo 50 za wafugaji katika kitongoji cha Kihonda Bwawani zimelalamikia hatua ya uongozi wa kijiji cha Sokoine cha kuweka vibao kwenye maeneo wanayoishi vinavyowataka kuondoka eneo hilo huku wakitaka kuleta wafugaji wengine kuishi kwenye eneo hilo kinyume na taratibu za sheria
Mwenyekiti wa tawi la Chama cha Mapinduzi ‘’CCM’’ katika Kitongoji cha Bwawani Jonas Koka alisema kuwa eneo hilo la ardhi walikuwa wakilimiliki muda mrefu na kuanza shughuli mbalimbali za kimaendeleo ikiwemo mashamba na ujenzi wa shule ya msingi kwa ajili ya kusomea watoto wao lakini wameshangazwa kuona vibao vinavyowataka kutofanya shughuli za maendeleo katika ene husika.
‘’wengi wetu ni wakulima na jamii ya kifugaji na tumekuwa tukijishughulisha na shughuli mbambalimbali ikiwemo kuchangia michango ya kimaendeleo katika kijiji cha Sokoine hivyo tunaishangaa serikali kutotujali na kututaka kuhama kwani siku zote walikuwa wapi au serikali ilikuwa haipo’’alisema Koka.
Naye Fidolina Komba,Sesilia Sangaya , John Olietieni na Peter Amo walisema kuwa woa kama wakazi wa kitongoji hicho wamekuwa wakiendesha shuhuli zao katika kitongoji hicho hivyo tunaiomba serikali kutusaidia kutatua kero hii kwani inaonekana kwamba uongozi wa kijiji cha Sokoine unawatetea wafugaji .
‘’sisi tunaiomba serikali iliangalie kero hii kwani endapo tutanyang’anywa ardhi hii tunayoishi sasa ambayo tuliikuta ni pori na kuanzisha makazi itakua ni uonevu kwani hatuna pengine pa kukimbilia na kwa nini watanzania wengine wapewa kipaumbele huku wengine wakinyanyaswa wakati wote ni raia wa tanzania"walisema .
Pia walilalamikia hatua ya uongozi wa serikali ya kijiji kuwachangisha michango bila utaratibu unaeleweka pamoja na kuwataka kuwalipia gharama za usafiri na chakula wanapofika maeneo hayo jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo yao.
naye Silvetus Yusuf na Mwalimu wa shule ya muda wanayosomea watoto wa kitongoji hicho walisema baada ya vibao hivyo watoto na wazazi wamekatishwa tamaa kuendeleza shule hiyo pamoja kwamba wazazi wamejitolea kujenga vyumba vya madarasa kwa zaidi ya shilingi milioni 20.0 kwa gharama zao na kuambiwa kusitisha ujenzi huo uliofikia hatua ya kuezeka.
walisema hali hiyo imesababisha watoto wengine kwenye kitongoji hicho kutosoma huku wengine kuolewa na kuona kutokana na shule kuwa umbali wa zaidi ya km 30 kutoka kitongojini hapo hadi shule ya msingi Sokoine.
Akizungumzaia suala hilo mkuu wa wilaya ya Mvomero Antony Mtaka alisema kuwepo kwa vibao hivyo kunalenga kuwasaidia watu wanaotapeliwa kununua maeneo katika eneo hilo huku serikali ya wilaya ikiwa bado haijaigawa ardhi hiyo kwa wananchi.
Hata hivyo alisema iwapo itabainika kuna wananchi wamevamia eneo hilo serikali haitasita kuwahamisha na kugawa maeneo hayo kwa mujibu wa sheria ya ardhi ya vijiji kwa kuwa imebainika kuwepo kwa baadhi ya watu kuwauzia watu ardhi kinyume na sheria.
‘’Hawa wananchi wanaolalamikia kwamba wanataka kuwaondoa eneo eneo hilo ni kweli kabisa na hii ni kutokana na wao kuvamia na kuanzisha makazi maeneo ambayo hayajapimwa na hivyo kuanza kujimilikisha ardhi bila ya kuishirikisha serikali au mamlaka zinazohusika na masuala ya ardhi’’alisema Mtaka.
Aidha alitoa onyo kwa wananchi Wilayani humo kujiepusha kurubuniwa kuuziwa ardhi au kujimilikisha pasipo uhalali kwani kufanya hivyo ni kuzidi kuibua migogoro ya ardhi isiyokwisha na kwamba iwapo mtu anahitaji ardhi ni vyema akafuata taratibu za kupata ardhi hiyo kisheria.
Kwa pande wake Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Jafari Majaliwa alisema kuwa migogoro mingi ya ardhi sehemu za vijiji au vitongoji inatokana na viongozi walioko huko na wanachi kujichukulia sheria mkononi na kujigawia ardhi kiholelea kinyume na sheria ya ardhi ya vijiji hivyo elimu inahitajika zaidi ili kuepukana na tatizo hilo sugu.
"Kuna baadhi ya viongozi wa vijiji wamekuwa wakighushi mihtasari na kuwagawia watu ardhi kinyume cha sheria na mihtasari hiyo tumeikamata kwenye baadhi ya vijiji ..... kwa kwenye ngazi ya vitongoji viongozi hawana mamlaka ya kugawa ardhi"alisema Majaliwa
No comments:
Post a Comment