Thursday, October 11, 2012

SERIKALI ANGALIENI MGOGORO KATI YA WAKULIMA NA MWEKEZAJI,MATETENI –KILOSA


WAKAZI 270 wa Kitongoji cha Matete, wilayani Kilosa, wameiomba Serikali kuupatia ufumbuzi mgogoro uliopo kati yao na mwekezaji wa Shamba la M 9, uliosababisha kubomolewa makazi yao na kuwafanya kuishi katika mazingira magumu.

Mwenyekiti mstaafu wa Serikali ya Kitongoji, John Kihelo na Katibu wa Kitongoji hicho, Thadeus Luanda, walisema tangu kubomolewa kwa nyumba zao Februari 16, mwaka huu na kupatiwa mahema 50 na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Halima Dendego, wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu.

Walisema mahema hayo kwa sasa yamekuwa machakavu, huku yakitoa harufu kali, jambo ambalo huwafanya kuishi katika mazingira yanayoweza kuwasababishia kupatwa na magonjwa, ikiwamo malaria, magonjwa ya tumbo na mengineyo.

Walisema wakati wakifanya jitihada mbalimbali katika kufuatilia suala hilo, waliweza kulifikisha kwa Rais Jakaya Kikwete, wakati wanachama wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) na wakulima wengine walipopata fursa ya kufikisha masuala yanayowahusu wakulima.

Walisema kutokana na kilio hicho, Rais Kikwete alimpa ofisa mmoja jukumu la kufuatilia suala hilo.

Walisema wakati mgogoro huo ukiwa katika mchakato wa kushughulikiwa, wakazi wa Kitongoji hicho wameendelea kupata vitisho vya mara kwa mara ambapo hivi karibuni walikatiwa umeme, ikiwamo mashine ya kusaga na kukoboa nafaka.

Alisema wakati wa mchakato huo, walimwelezea Mkuu wa Wilaya hiyo, Elias Tarimo, lakini bado kumekuwa na vitisho vya mara kwa mara, huku wakielezwa kuhamishwa na mwekezaji wa eneo hilo wa sasa, anayefahamika kwa jina moja la Rugarabamu.

Walisema awali shamba hilo lilikuwa likimilikiwa na aliyekuwa Katibu wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye ni Timoth Opiyo, ambapo alizungumza na wakazi wa kitongoji hicho.

Walisema mwaka 2010 wakati nyumba zao zilipokumbwa na mafuriko, uongozi wa wilaya na mkoa uliagiza wananchi hao kuhamia maeneo ya mwinuko, ikiwamo eneo hilo lililokuwa kama limetelekezwa kutokana na kuwa pori.

Walisema wakulima hao waliendelea na shughuli zao za kilimo na kufuga, lakini Februari 16, mwaka huu, askari polisi wakiwa na vijana wengine na mtu mmoja aliyekuwa akiishi eneo hilo aliyetambulika kwa jina la Odede, huku wakiwa na greda, walianza kubomoa nyumba zao.

Walisema pamoja na kuzuiwa na askari wa Kituo cha Polisi Dumila, lakini walishangazwa na hatua ya askari waliohusika katika ubomoaji huo.

Akizungumzia malalamiko hayo, Tarimo, alikiri kupokea tatizo hilo na kuahidi kulishughulikia, huku akiagiza wananchi hao kuendelea kubaki katika eneo hilo hadi suala hilo litakapopatiwa ufumbuzi.

Aidha, aliwataka watu wanaopatiwa ardhi na Serikali kwa ajili ya kuwekeza ni vyema kama ilivyokusudiwa kuliko kuitelekeza.

Alisema wanaendelea kufanya tathimini ya mashamba yaliyochukuliwa na watu kwa lengo la kuwekeza lakini hayaendelezwi, huku wengine wakitumia kinyume na malengo waliyoombea.

Naye, Ofisa Utetezi na Ushawishi wa MVIWATA, Thomas Laizer, alimwambia Tarimo kuwa hali ni mbaya baina ya wakulima na wafugaji kutokana na matukio yanayojitokeza na kuripotiwa katika vyombo vya sheria.

Alisema iwapo hatua za makusudi hazitachukuliwa kwa pande hizo mbili, hali inaweza kuwa mbaya kutokana na wakulima kuchoshwa na ukatili wanaofanyiwa.

No comments:

Post a Comment